Mahakama ya Kenya Kutoa Uamuzi Kuhusu Ombi la Kuzuwia Kuondolewa kwa Naibu Rais Gachagua

Mahakama nchini Kenya inatarajiwa kutoa uamuzi siku ya Jumanne kuhusu kesi ya mwisho ya kutaka kusitisha mjadala wa Seneti na kupiga kura kuhusu kuondolewa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Katika hatua ya kihistoria wiki jana, baraza la chini la bunge, Bunge la Kitaifa, lilipiga kura kwa wingi kumshtaki Gachagua kwa tuhuma 11 zikiwemo za ufisadi.

Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua

Gachagua, ambaye ana umri wa miaka 59, amekanusha madai yote na ataendelea kuhudumu katika nafasi yake hadi Bunge la Seneti litakapoamua kuidhinisha kuondolewa kwake.

Gachagua aliwasilisha pingamizi katika mahakama hiyo kusitisha kesi ya baraza la juu iliyopangwa Jumatano na Alhamisi, akisema kuwa kuondolewa kwake hakukuwa na haki.

Jaji wa Mahakama Kuu Enock Chacha Mwita atatoa uamuzi kuhusu kesi hiyo saa nane na nusu.

Hiyo ni mojawapo ya kesi nyingi za kimahakama ambazo zimewasilishwa kupinga kuondolewa madarakani, ikiwa ni kesi ya kwanza ya aina yake dhidi ya naibu rais tangu uwezekano huo kuanzishwa katika katiba ya Kenya iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.

Mnamo Jumatatu, Jaji Mkuu Martha Koome aliteua benchi ya majaji watatu kusikiliza na kuamua kesi ya kuunganisha maombi sita kati ya hayo.

Gachagua, mfanyabiashara kutoka kabila kubwa zaidi nchini Kenya, Wakikuyu, alikabiliana na kashfa za awali za ufisadi na kuwa naibu kiongozi kama mgombea mwenza wa Rais William Ruto katika uchaguzi uliopiganwa kwa karibu Agosti 2022.

Lakini katika wiki za hivi majuzi, amelalamika kutengwa na rais na alikuwa akishutumiwa kwa kuunga mkono maandamano ya kupinga serikali yaliyoongozwa na vijana yaliyozuka mwezi Juni.

Gachagua, ambaye anadaiwa kumtishia jaji kati ya mashtaka yake ya kumtimua, Jumapili alisema aliweka matumaini yake kwa idara ya mahakama.

“Mimi ni muumini wa uhuru wa mahakama. Nina hakika kwamba mahakama zitatumia mamlaka ya mahakama na kulinda na kuzingatia katiba na matakwa ya watu,” alisema wakati wa ibada ya kanisa.
Ruto hajazungumzia hadharani kuhusu kutimuliwa kwa Naibu wake Rigathi Gachagua.

Kuondolewa kutahitaji kuungwa mkono na angalau theluthi mbili ya maseneta ili kupitishwa.