Watu zaidi ya 10 wameripotiwa kufariki dunia kufuatia mlipuko wa lori la mafuta katika kitongoji cha Kigoogwa kwenye viunga vya kaskazini mwa jiji, kwenye barabara inayounganisha Kampala na mji wa kaskazini wa Gulu, polisi walisema.
“Waathiriwa waliteketea kiasi cha kutoweza kutambuliwa,” polisi walisema. Wingu la moshi mweusi lilipaa kutoka eneo la tukio.
Kulingana na ripoti za polisi, lori hilo la mafuta lilipinduka karibu saa 1500 saa za eneo na kusababisha “watu kadhaa kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa”.
Video za kusikitisha zilizotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa X zilionyesha lori hilo la mafuta likiwa limelala ubavu huku baadhi ya wakazi wakilikimbilia wakiwa wamebeba mikebe ili kuchota mafuta.
Kadhalika katika video nyingine, moto mkubwa ulionekana ukiteketeza lori hilo na baadhi ya nyumba zilizokuwa karibu.