Kikosi cha waokoaji wa Uturuki kilianza msako wa kina katika gereza maarufu la Saydnaya nchini Syria siku ya Jumatatu, hii ni kulingana na msemaji wa shirika la kudhibiti majanga la Uturuki la AFAD ambaye alizungumza na shirika la Habari la AFP.
Jela hiyo iliyo kaskazini mwa Damascus, imekuwa ishara ya ukiukwaji wa haki za ukoo wa Assad, haswa tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria vilipoibuka mnamo 2011.
Wafungwa waliokuwa wakishikiliwa ndani ya jengo hilo, ambalo lilikuwa eneo la kunyongwa bila ya mahakama, kuteswa na kutoweka kwa lazima, waliachiliwa mapema wiki iliyopita na waasi waliomtimua kiongozi wa Syria Bashar al-Assad mnamo Desemba 8, 2024.
AFAD imesema imetuma timu ya karibu watu 80 kufanya operesheni ya kuwasaka na kuwaokoa ili “kuwapata watu wanaodhaniwa kuwa wamenaswa katika jela ya kijeshi ya Sadnaya”, huku mkurugenzi wake akitarajiwa kutoa mkutano na waandishi wa habari nje ya gereza hilo kuhusu dhamira yake, alisema msemaji Kubilay Ozyurt akiliambia shirika la Habari la AFP.
Jengo hilo linafikiriwa kushuka ngazi kadhaa chini ya ardhi, na hivyo kuzua shaka kuwa wafungwa zaidi wanaweza kuzuiliwa katika seli ambazo bado hazijagunduliwa.
Lakini Muungano wa Wafungwa na Watu Waliopotea wa Gereza la Saydnaya (ADMSP), wanaamini kuwa uvumi huo hauna msingi.
Kulingana na ripoti kutoka shirika la habari la jimbo la Anadolu, ni kwamba AFAD ilisema timu hiyo, ambayo ni maalumu katika shughuli “nzito” za utafutaji na uokoaji mijini, itafanya kazi na “vifaa vya juu vya utafutaji na uokoaji”
Jela hilo lilipekuliwa kwa kina na wafanyakazi wa dharura wa Kofia Nyeupe nchini Syria lakini walimaliza shughuli zao siku ya Jumanne, wakisema hawakuweza kupata wafungwa wengine zaidi.
Waokoaji wametoboa mashimo kwenye kuta kuchunguza uvumi wa makazi ya siri ya kukosekana kwa wafungwa, lakini hawakupata chochote, na kuacha maelfu ya familia wakiwa wamekata tamaa — jamaa zao pengine wamekufa na huenda hawapatikani kamwe.
ADMSP ilisema waasi waliwaachilia zaidi ya wafungwa 4,000 kutoka Saydnaya, ambayo Amnesty International imeelezea kama “kichinjio cha binadamu”.
Shirika hilo lenye makao yake makuu kusini mwa Uturuki, linaamini zaidi ya wafungwa 30,000 walifia huko kutokana na kunyongwa, kuteswa, njaa au ukosefu wa huduma za matibabu kati ya 2011 na 2018.