Katika hatua muhimu kwenye mgogoro wa muda mrefu wa Gaza, Israel na kundi la Hamas wamefikia makubaliano ya kihistoria ya kusitisha mapigano, yaliosimamiwa na Qatar. Viongozi wa ulimwengu wamepongeza hatua hiyo.
Mwanaume akipunga bendera za Palestina huku Wapalestina wakishangilia habari za makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel, mjini Deir Al-Balah, katikati mwa Ukanda wa Gaza, Januari 15, 2025.
Makubaliano hayo, yaliyotangazwa Jumatano jioni na Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, yanajumuisha kuwachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina walioko katika magereza ya Israel.
Usitishaji huu wa vita unatarajiwa kuanza Jumapili na utaendelea kwa siku 42, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa pande hizo kusitisha mapigano tangu vita vilipoanza tena Gaza miezi 15 iliyopita.
“Makubaliano haya yanatoa matumaini kwa raia wa pande zote ambao wamepitia mateso makubwa,” alisema Al Thani, akihimiza pande zote kudumisha utulivu wakati wa utekelezaji wa makubaliano hayo.
Kwa mujibu wa Rais wa Marekani Joe Biden, usitishaji huu wa vita ni sehemu ya mpango wa hatua tatu unaolenga kufanikisha kumalizika kwa mgogoro huo kwa njia ya kudumu.
Akizungumza katika Ikulu ya White House, Biden alieleza kuwa hatua ya kwanza ni kipindi cha wiki sita cha kusitisha kabisa mapigano, kuondolewa kwa vikosi vya Israel kutoka maeneo yenye wakazi wengi Gaza, na kuachiliwa kwa mateka walioko mikononi mwa Hamas.
Katika kipindi hiki, mazungumzo yataendelea kwa lengo la kufanikisha hatua ya pili ya kumaliza vita kabisa.
“Usitishaji huu wa mapigano siyo tu muda wa kupumzika; ni hatua ya kuelekea amani ya kudumu,” alisema Biden, akisisitiza msaada wa Marekani katika kufanikisha mpango huu.