Mbunge wa Kenya amtaka Rais Samia kuelezea mbona alizuiliwa Kuingia Tanzania

Mbunge wa Kenya Babu Owino amemwandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akitaka kujua mbona alizuiliwa kwa muda kuingia Tanzania.

Katika barua yake ya  Februari 3 2025, mbunge huyo alielezea jinsi alivyonyimwa kibali cha kuingia Tanzania mwezi  Disemba mwaka 2024.

“Ninaweka ombi hili maalum ofisini kwako ili kunifafanulia kwa maandishi sababu za kutoruhusiwa kuingia Tanzania kwa ajili ya biashara, au kama mwakilishi wa watu wa Kenya, au kama rafiki wa watu wa Tanzania na kwa sababu nyingine yoyote halali,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, Serikali ya Tanzania ilimzuilia kwa takriban saa 3 mnamo Desemba 2024 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kuwasili Tanzania na kukatanzwa kuingia.

Kwenye uwanja wa ndege, wafanyakazi walimjulisha Babu Owino kuwa jina lake lilikuwa kwenye orodha ya watu wasio na kubalika  nchini Tanzania.

“Naandika ili nikuelezee kwamba nilipotembelea Tanzania hivi karibuni Desemba 2024 baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, maafisa wenu wa uhamiaji walikataa pasipoti yangu na kuniarifu kwa kawaida kuwa niko kwenye orodha ya watu wasio na kubalika nchini Tanzania,” Owino aliandika.

“Kwa kukiuka kabisa haki zangu za uhuru wa kutembea, walinikamata kwa muda katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.” Aliendelea kusema Babu Owino

Matokeo haya yasiyotarajiwa yalimfanya mbunge huyo wa Kenya kulalamikia ukiukaji wa haki yake sio tu kama raia wa Afrika Mashariki bali pia kama mwakilishi wa Bunge la Kenya ambalo linampa haki ya kuingia Tanzania.” Mimi ni raia wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hasa Kenya, kwa jambo hilo. Mimi ni mbunge wa Bunge la Kenya, ambalo linawakilishwa kihalali katika EALA, ambalo kiti chake kiko Tanzania,” barua yake iliendelea.

“Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) unahakikisha haki za watu za kuingia na kutoka katika mataifa baada ya kufuata mchakato unaofaa, ambao nilifanya.”

Aidha, alisema kuwa Mkataba wa Afrika Mashariki na Kanuni za Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Free Movement of Persons) zinatoa uhuru wa kusafiri kwa raia wa nchi washirika.

“Mwisho, Kenya, kama taifa huru, inatoa pasipoti za kusafiri kwa raia wake, ambazo zinatambuliwa na mataifa mengine chini ya sheria za kimataifa. Haki hizo zote na uhuru wa msingi unanihusu mimi kama raia wa sayari hii,” alihitimisha.