Mtangazaji nguli wa Kenya Leonard Mambo Mbotela amefariki

Tasnia ya habari nchini Kenya inaomboleza kifo cha mwanahabari nguli Leonard Mambo Mbotela aliyefariki akiwa na umri wa miaka 85.

Mbotela amefanya kazi ya uandishi wa habari kwa zaidi ya miongo mitano, lakini tukio lililoandikisha historia katika maisha yake ni jaribio la mapinduzi ya mwaka 1982 ambapo baadhi ya wanajeshi wakati huo walitaka kumuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa wakati huo Danie Arap Moi.

 

Wanajeshi hao waasi walimchukua nyumbani kwake na kumpeleka katika kituo cha redio cha Sauti ya Kenya VOK na kumlazimisha atangaze kuwa serikali ya Rais Moi imepinduliwa.

Pia atakumbukwa kwa kipindi chake cha Jee Huu ni Ungwana alichokifanya kwa ucheshi uliowakonga mioyo wasikilizaji wake na ambacho kilopeperushwa hewani kwenye Redio na ba baadaye kwenye Televisheni ya Shirika la Utangazaji la Kenya KBC.

Kipindi hicho kilianzishwa mnamo 1966 na kilipeperushwa hewani kwa takriban miaka 55.

Mbotela alizaliwa mnamo Mei, 29 mwaka 1940 na hadi kifo chake, alikuwa na umri wa miaka 85.

Alizaliwa katika mji wa Frere  huko Mombasa na kusomea katika shule ya msingi ya Frere na kisha akajiunga na shule ya upili ya Kitui.

Baada ya kumaliza masomo, Mbotela katika mahojiano yaliyopita aliiambia KBC kuwa alienda kutafuta ajira mjini Nakuru.

Ingawa alifanya hivyo, ari yake ya utangazaji ilikuwa ikimrindima akilini.

 

Ni wakati akiwa mjini Nakuru ambapo kipaji chake cha uanabari kilipaliliwa baada ya kujiunga na gazeti la Baraza lililochapishwa mjini humo kama Ripota.

 

“Ingawa nilikuwa Nakuru, nilitamani ningekuja jijini Nairobi na kujiunga na VoK wakati huo, ” Mbotela alinukuliwa akisema wakati akihojiwa kwenye kipindi cha “Legends Edition” na Catherine Kasavuli, mtangazaji mwingine nguli ambaye pia ametangulia mbele za Mungu.

 

Tamanio ambalo lilikuja kutimia baadaye alipojiunga na VoK.

Alifahamika sana kutokana na kipindi chake cha “Je, Huu ni Uungwana” kilichopeperushwa kwenye idhaa ya redio na runinga ya KBC.

Kando na kuwa mtangazaji, Mbotela pia alikuwa mwimbaji hodari.