Je, maandamano eSwatini yanaashiria mwisho wa uongozi wa kifalme?

Maandamano yamejumuisha wanafunzi, mashirika ya wafanyakazi na asasi za serikali wamekuwa wakidai mageuzi ya siasa.

0
Mswati III. Mfalme wa eSwatini

Taifa la eSwatini ambalo awali lilijulikana kama Swaziland limekumbwa na maandamano na ghasia sasa kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Waandamanji hao wakijumuisha wanafunzi wa shule za msingi na za upili,mashirika ya wafanyakazi na asasi za serikali wamekuwa wakidai mageuzi ya siasa.

eSwatini ni taifa dogo la Afrika kusini limepakana na mataifa ya Msumbiji na Afrika Kusini. Ni taifa la mwisho barani Afrika kuongozwa na mfalme. Kama kiongozi na mfalme mwenye nguvu, Mfalme Mswati III anajukumu la kuteua viongozi ikiwa ni kumteua Waziri Mkuu, viongozi wengine wakuu serikalini pamoja na viongozi wakuu wa kitamaduni.

Nchi hiyo ilifahamika kama Swaziland hadi mwaka wa 2018, ilipobadili jina na kuanza kutumia eSwatini, jina linalotokana na jina la mfalme Mswati.

eSwatini ni mshirika wa miungano ya SADC, AU, Jumuia ya Madola na Umoja wa Mataifa.

Kiongozi wa sasa wa Ufalme wa eSwatini ni Mswati III, alitawazwa kuwa mfalme wa taifa hilo la Afrika Kusini akiwa na umri wa miaka 18 baada ya kifo cha babake Mfalme Sobhuza 11 tarehe 25 Aprili 1986.

Alipotawazwa kuwa mfalme akiwa na umri wa miaka 18, alikuwa kiongozi mchanga zaidi duniani kushikilia wadhfa wa uongozi.

Mswati III ana wake 15, wengi wao akiwa amewachagua katika sherehe za kila mwaka za Reed Dance.

Baadhi ya wake wa Mswati III

eSwatini ni kati ya mataifa ambayo hujivunia na kudumisha tamaduni zao.Moja ya tamaduni hizo ni densi ya kila mwaka ya Reed Dance, sherehe hizo hushirikisha mabinti bikra pekee,Mswati huchagua bibi kila mwaka katika sherehe hiyo.

Kando na kuwa amekuwa uongozini kwa muda mrefu na ameweka mageuzi ya siasa kama vile kuunda katiba mpya iliyoruhusu uhuru wa kusema na kujumuika na uhuru wa vyombo vya habari, wengi wa wanaharakati nchini humo wanasema mabadiliko hayo hayatoshi na wanataka mageuzi zaidi.

Uongozi wa Mfalme Mswati III umekumbwa na mizozo ya kisiasa katika siku za hivi karibuni.

Mnamo Juni 2021, maandamono makubwa yalizuka nchini eSwatini kupinga uongozi wa ubabe, ukandamizaji wa upinzani na matumizi mabaya ya fedha. Inadaiwa kuwa maandamano hayo yalimfanya Mswati kutorokea Afrika Kusini usiku wa 28-29 madai yaliyopingwa na kaimu Waziri mkuu Themba Masuku.

Kwa mwezi mmoja sasa maandamano mapya yamekuwa yaiendelezwa na wanafunzi wa shule za msingi na za upili, ambao pia wamekuwa wakidai mageuzi ya kisiasa. Maandamano hayo ya wanafunzi yamesababisha takriban shule 80 kufungwa nchini humo.

Wanafunzi hao wanadai mifumo bora ya elimu pamoja na elimu ya bure, wakisema masomo yamekuwa ghali nchini humo na kuwazuia wanafunzi wengi kuendeleza kisomo chao.

Jumatano ya 13 Okotoba, vurugu na machafuko yalitanda katika mji wa Malkerns ambako wanaharakati na asasi tofauti za serikali wamekuwa wakidai mabadiliko ya siasa na uongozi wa demokrasia nchini humo.

Watu kadhaa wamejeruhiwa kwenye maandamano hayo ambayo pia yanatumika kuishinikza serikali kuachiwa kwa wanasheria wawili wanaozuiwa na polisi kwa kuongoza maandamano ya kudai uongozi wa demokrasia. Takriban watu 27 wameuawa kwenye makabiliano na polisi.

Waandamanaji, asasi za serikali na wanaharakati wanadai uongozi wa demokrasia na kupunguzwa kwa nguvu za mfalme. Wamekuwa pia wakipinga matumizi mabaya ya fedha ambapo Mswati III na wake zake 15 na watoto 23 wanaishi maisha mazuri na wananchi wengi wakiishi kwa uchochole.

Maandamano yalizuka mapema mwezi Juni, na hata baada ya polisi na jeshi kutumwa kuzima maandamao hayo, waandamanaji, wanaharakati na asasi za serikali wanaendelea kujitokeza kudai uongozi bora nchini humo.

Watu wengi wanaendelea kujitokeza na kujiunga na maandamano na sasa swali kwenye vinywa vingi ni, je huu ndio mwisho wa uongozi wa Kifalme nchini eSwatini?

Mswati III wa eSwatini

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted