Tuzo ya Nobel ni tuzo ya kimataifa inayotolewa kila mwaka tangu ilipozinduliwa rasmi mwaka wa 1901 kusheherekea hatua kubwa zinazopigwa katika vitengo vya Fiziolojia,Kemia,Saikolojia, Dawa , Fasihi na Amani.
Tangu tuzo hizo zilipozinduliwa, watu 800 kutoka mataifa tofauti kote duniani wameshinda tuzo ya Nobel katika vitengo hivyo tofauti.
Watu kadhaa kutoka Afrika wameshinda tuzo ya Nobel katika vitengo vitano kati ya sita vya Nobel ikiwa ni katika Amani, Fizikia,Saikolojia, Fasihi na Kemia.
Mwafrika wa kwanza kushinda tuzo ya Nobel alikuwa ni Albert Luthuli mnamo mwaka wa 1960, aliposhinda tuzo ya Amani ya Nobel. Inkosi Albert John Luthuli alikuwa mwanaharakati, mwalimu na mwanasiasa kutoka Afrika Kusini. Alipewa tuzo ya Nobel ya Amani kwa kupinga ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.
Nelson Mandela, rais wa kwanza mwafrika Afrika Kusini pia alishinda tuzo ya Amani ya Nobel kwa kupinga kwa amani ubaguzi wa rangi Afrika Kusini. Alipewa Tuzo ya Amani ya Nobel mnamo 1993 pamoja na Rais F.W De Klerk. Desmond Tutu, kasisi na mpinzani wa uongozi wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini alishinda tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 1984.
Viongozi wengine wa Afrika kushinda tuzo ya Nobel ni pamoja na Anwar Sadat aliyekuwa rais wa Misri ,alishinda tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 1978. Rais wa zamani wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf alishinda tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 2011 pamoja na Leymah Gbowee pia kutoka Liberia.
Kutoka taifa la Afrika Magharibi Ghana, Kofi Annan alishinda tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 2001. Kofi Atta Annan alihudumu kama Katibu Mkuu wa saba wa Umoja wa Mataifa kutoka mwaka wa 1997 hadi 2006.
Kofi Annan anakumbwa zaidi nchini Kenya ambako aliwapatanisha Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga baada ya uchaguzi mkuu tata wa 2007 uliosababisha mapigano na mauaji.
Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia ni kiongozi mwingine ambaye ameshinda tuzo ya Amani ya Nobel akiwa amashinda tuzo hiyo mwaka wa 2019.
Wengine kutoka Afrika kushinda tuzo ya Amani ya Nobel ni daktari na kasisi Denis Mukwege kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo mwaka wa 2018 kwa juhudi zake za kutibu wanawake waliobakwa na makundi ya magaidi nchini DR Congo.
Mwanamke wa kwanza mwafrika kushinda tuzo ya Nobel ni Wangari Maathai. Maathai alishinda tuzo ya Amani ya Nobel mwaka wa 2004, akishinda tuzo hiyo kwa juhudi zake za kutunza mazingira.
Mwafrika wa kwanza kushinda tuzo ya Nobel katika Fasihi alikuwa mwandishi wa riwaya kutoka Nigeria, Wole Soyinka.Akinwande Oluwole Babatunde Soyinka alishinda tuzo hiyo mwaka wa 1986. Soyinka ni mwandishi wa riwaya, tamthilia na mashairi.
Hivi maajuzi mwandishi mwingine kutoka Afrika kushinda tuzo ya Nobel katika Fasihi alikuwa ni Abdulrazak Gurnah.
Mwandishi wa riwaya kutoka Zanzibar alikuwa mshindi wa hivi maajuzi mwafrika kushinda tuzo ya Nobel katika Fasihi 2021 baada ya Wole Soyinka kushinda mwaka wa 1986.
Tuzo ya Nobel inatolewa na taasisi ya Uswizi ya Nobel na ina thamani ya pesa za Uswizi crowns milioni 10.