Maandamano ya kudai haki kwa mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang’ yalivurugwa Jumanne na kundi la watu wanaodaiwa kuwa wahuni waliowasili kwa pikipiki katikati mwa jiji la Nairobi.

Wakiwa wamevalia mavazi mazito na kufunika nyuso zao, wahuni hao walionekana wakipita kwenye barabara kuu kama Tom Mboya, Moi Avenue na Kenyatta Avenue, huku wakisababisha taharuki kwa waandamanaji na wakaazi wa jiji. Mashuhuda wanasema baadhi ya watu hao walikuwa wamejihami kwa marungu na visu, na waliripotiwa kuwahangaisha raia na waandamanaji.
Wakati huo huo, waandamanaji walikuwa wamekusanyika nje ya jengo la Nation Centre kwa sala kabla ya kuanza maandamano yao. Polisi walitumia vitoa machozi kuwatawanya, hali iliyozua taharuki na kusababisha baadhi ya biashara kufungwa kwa hofu ya uporaji, kama ilivyotokea wiki iliyopita.
Maandamano hayo yaliendelea licha ya vurugu, huku waandamanaji wakiimba nyimbo za kizalendo na kushikilia mabango yaliyokuwa yakimtaka Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat ajiuzulu kabisa. Ingawa alitangaza kujiondoa kwa muda Juni 16 ili kupisha uchunguzi, baadhi ya waandamanaji wamesisitiza kuwa hatua hiyo haitoshi.
Maandamano kama haya pia yameripotiwa katika miji mingine kama Mombasa, ambapo raia wanadai haki na kukomeshwa kwa mauaji ya kiholela na ukatili wa polisi.