Museveni Kutetea Tena Kiti Cha Urais 2026

Rais wa muda mrefu wa Uganda, Yoweri Museveni, atawania tena urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka 2026, chama chake tawala kimethibitisha Museveni mwenye umri wa miaka 80, ambaye amekuwa madarakani kwa karibu miongo minne, alitarajiwa kwa kiasi kikubwa kuwania muhula mwingine wa uongozi wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Museveni Kutetea Tena Kiti Cha Urais 2026

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya chama cha National Resistance Movement (NRM), chama hicho kilisema kuwa Museveni “amewasilisha nia ya kutetea nafasi ya Mwenyekiti wa NRM na kuwa mgombea urais wa chama katika uchaguzi wa 2026.”

Museveni, ambaye hapo awali alisifiwa kwa msimamo wake wa utawala bora baada ya kuingia madarakani kama kiongozi wa waasi mwaka 1986, ameendelea kukandamiza wapinzani kwa miaka ya karibuni na kubadilisha katiba mara kadhaa ili kujiruhusu kuendelea kugombea.

Yoweri Museveni akiapishwa kuwa Rais wa Uganda, Januari 29, 1986

Taarifa ya chama hicho imekuja wakati ambapo wapinzani wake wakuu, akiwemo mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa maarufu, Bobi Wine (jina halisi Robert Kyagulanyi), naye ametangaza rasmi nia ya kugombea urais mwaka 2026.

Bobi Wine alishindwa na Museveni katika uchaguzi wa 2021, uchaguzi ambao ulighubikwa na tuhuma za udanganyifu mkubwa na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola.

Wine amekamatwa mara kadhaa, huku mwana wa Museveni na anayechukuliwa kama mrithi wake wa kisiasa, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, akitoa vitisho vya wazi dhidi yake kupitia mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kutishia kumkata kichwa.

Mpinzani mwingine wa muda mrefu wa Museveni, Kizza Besigye, alitekwa mwaka jana akiwa nchini Kenya na kurejeshwa kwa nguvu Uganda, ambako sasa anakabiliwa na hukumu ya kifo kwa kosa la uhaini.

Mashirika mbalimbali ya haki za binadamu duniani yamepinga vikali mashtaka hayo, yakisema ni ya kisiasa. Mke wa Besigye, Winnie Byanyima, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, alisema kuwa mumewe anashikiliwa “kwa sababu za kisiasa”.

Aliongeza: “Anahukumiwa kwa sababu ameamua kuwania nafasi ya uongozi kupitia uchaguzi wa kidemokrasia.”