Mahakama Tanzania Yapiga Marufuku Urushaji ‘LIVE’ wa Ushahidi wa Mashahidi wa Siri Katika Kesi ya Lissu

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imekubali ombi la Jamhuri la kuzuia urushaji, utangazaji na usambazaji wa moja kwa moja wa mwenendo wa mashahidi wa siri katika kesi ya uhaini inayomkabili mwenyekiti wa chama cha upinzani cha CHADEMA, Tundu Lissu.

Mahakama Tanzania Yapiga Marufuku Urushaji ‘LIVE’ wa Ushahidi wa Mashahidi wa Siri Katika Kesi ya Lissu

Uamuzi huo umetolewa leo na mahakama hiyo baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hoja ukitaka kulindwa kwa usalama na utambulisho wa mashahidi wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Kwa mujibu wa maamuzi ya mahakama, marufuku hiyo inahusu vyombo vyote vya habari na watu binafsi, na itaendelea hadi mahakama itakapotoa uamuzi tofauti.

Hakimu anayesikiliza shauri hilo amesema kwamba yeyote atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria.

Tundu Lissu, ambaye pia ni wakili na mwanasiasa maarufu nchini Tanzania, anakabiliwa na mashtaka ya uhaini yanayohusiana na matamshi na vitendo vinavyodaiwa kuhatarisha usalama wa taifa.

Kesi hiyo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu na watanzania pamoja na jamii ya kimataifa, ikizingatiwa nafasi yake katika siasa za upinzani nchini humo.

Hata hivyo, baadhi ya wadadisi wa masuala ya haki za binadamu wameeleza wasiwasi wao kuhusu uwazi wa mwenendo wa kesi hiyo, wakisema kuwa hatua hiyo inaweza kuathiri haki ya umma kupata taarifa.