Maandamano makubwa yamezuka katika miji kadhaa ya Indonesia kufuatia kifo cha Affan Kurniawan, dereva wa pikipiki za usafirishaji (ojek), aliyeuawa baada ya kugongwa na gari la polisi la kikosi cha Brimob wakati wa vurugu nje ya bunge mnamo Alhamisi.

Waandamanaji, wakiwemo madereva wa ojek waliovaa jaketi zao za kijani, walikusanyika nje ya makao makuu ya polisi wakipiga kelele za “Muuaji! Muuaji!” huku wakirusha fataki na mawe. Polisi walijibu kwa kurusha mabomu ya machozi na kutumia magari ya maji kuwatawanya.

Rais Prabowo Subianto alieleza masikitiko yake na kuagiza uchunguzi wa kina, akiahidi kuwawajibisha maafisa waliohusika. Familia ya Kurniawan imethibitisha kuwa hakuwa sehemu ya maandamano, bali alikuwa akifanya kazi ya usafirishaji wakati wa tukio hilo.

Maandamano haya pia yamechochewa na hasira kuhusu posho kubwa za wabunge, kupunguzwa kwa bajeti ya elimu, na hali ngumu ya kiuchumi. Miji kama Surabaya, Medan, na Bandung pia imeshuhudia maandamano yenye vurugu, huku baadhi ya vituo vya polisi vikichomwa moto.
Wito wa haki kwa Affan Kurniawan umeenea mitandaoni, huku hashtag #PolisiPembunuh ikitrend. Wanaharakati na vyama vya wafanyakazi wanataka mabadiliko ya haraka katika utendaji wa vyombo vya usalama na uwajibikaji wa serikali.