
Mshtakiwa wa kesi ya uhaini, Tundu Lissu leo ameibua pingamizi jingine katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, akipinga kupokelewa kwa taarifa ya uchunguzi wa kitalaamu kama kielelezo katika kesi yake.
Pingamizi hilo limewasilishwa muda mfupi baada ya Mahakama kutoa uamuzi wa pingamizi la awali, ambapo Lissu alipinga upokelewaji wa vielelezo vya video vilivyohifadhiwa katika Flash Disk na Memory Card.
Katika uamuzi huo wa awali, Mahakama ilikubaliana na hoja ya Lissu kwamba shahidi aliyeleta vielelezo hivyo, Mkaguzi wa Polisi Samwel Kaaya (39), hakuwa mtaalamu wa video bali wa picha mnato, hivyo vielelezo hivyo havikupokelewa.
-Pingamizi Jipya-
Akitoa hoja ya pingamizi jipya, Lissu ameiambia Mahakama kuwa kwa mujibu wa vifungu vya 216, 217, 218, 219 na 220 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), shahidi anayetakiwa kuwasilisha taarifa za uchunguzi wa kitalaamu ni yule aliyetajwa kisheria katika vifungu hivyo.
Lissu amesema shahidi Kaaya amejitambulisha kama mtaalamu wa picha mnato si mtaalamu wa uchunguzi wa video, hivyo hana sifa za kuwasilisha taarifa hiyo kama kielelezo.
“Kwenye kielelezo anachotaka kuwasilisha, shahidi Kaaya amesema wazi kwamba yeye ni mtaalamu wa picha mnato kwa mujibu wa kifungu cha 202(1) cha CPA ya mwaka 2022, ambacho sasa ni kifungu cha 216(1) katika marejeo ya mwaka 2023. Kifungu hiki kinahusu watalaamu wa picha mnato pekee, si wa video au uchunguzi wa taarifa za kielektroniki,” alisema Lissu.
Aidha, Lissu amedai kuwa uteuzi wa shahidi huyo kama mtaalamu haukufuata taratibu za kisheria kwani ulitolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) badala ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kama sheria inavyotaka.
“Tangazo la Serikali lililomteua shahidi huyo, namba 799 la mwaka 2020, lilitolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo Profesa Adelardus Kilangi, na si DPP. AG hana mamlaka ya kufanya uteuzi wa mtaalamu wa aina hiyo,” alisisitiza Lissu.
Kwa mujibu wa Lissu, hati hiyo ya uchunguzi haina kiambatanisho chochote cha picha (photographic print), jambo linaloonyesha shahidi huyo hana mamlaka ya kuwasilisha taarifa hiyo.
Kwa upande wa mashtaka, Wakili wa Serikali Job Mrema alipinga pingamizi hilo akidai kwamba kielelezo kinachoombwa kupokelewa ni tofauti na vile vilivyokataliwa awali (Flash Disk na Memory Card).
“Ni kweli Mahakama ilitupilia mbali vielelezo vya Flash Disk na Memory Card, lakini kielelezo kinachoombwa sasa ni taarifa ya mtaalamu, ambayo ni nyaraka tofauti kabisa,” alisema Mrema.
Akaongeza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 216 cha CPA, shahidi anayeleta taarifa kama hiyo ndiye mtaalamu anayezungumziwa kisheria, hivyo Mahakama inapaswa kukubali upokelewaji wa kielelezo hicho.
Akijibu hoja hizo, Lissu alisema hoja ya Jamhuri haina mashiko kwani taarifa inayotaka kuwasilishwa inatokana moja kwa moja na vielelezo ambavyo Mahakama tayari imevikataa.
“Ripoti hii haiwezi kusimama peke yake bila Flash Disk na Memory Card, kwa sababu taarifa yenyewe inachambua kilichomo ndani ya vifaa hivyo. Mahakama ilishavikataa, kwa hiyo na ripoti hii pia haiwezi kupokelewa,” alisema Lissu.
Aidha, alieleza kuwa hoja ya Jamhuri kuhusu utofauti wa nyaraka hizo haina msingi kwani zote ni vielelezo vinavyohusiana.
“Ni kweli Flash Disk ni tofauti na karatasi, lakini ripoti hii inategemea kile kilichomo ndani ya Flash Disk na Memory Card. Kimoja kikikosa uhalali, kingine hakiwezi kusimama,” alihitimisha Lissu.
Kesi imeahirishwa mpaka kesho Oktoba 23, 2025 kwa ajili ya kutolewa uamuzi mdogo