Kesi Ya Uhaini Ya Tundu Lissu Kuendelea Baada Ya Uchaguzi Mkuu

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeahirisha kesi ya uhaini nayomkabili Tundu Lissu hadi tarehe 3 Novemba 2025, baada ya upande wa mashtaka kuomba muda zaidi kwa ajili ya kuandaa mashahidi wanaofuata kwa kua leo wamekosa shahidi wa kumleta mahakamani hapo baada ya shahidi wao tatu kumaliza kutoa ushahidi hapo jana.

Kesi ya Lissu: Jamhuri Wakosa Shahidi, Kesi Yaahirishwa Hadi Novemba 3,2025

Akizungumza mbele ya Jopo la Majaji,  watatu wakiongozwa na Jaji  Dastan Ndunguru akisaidiana na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde Wakili wa Serikali  Renatus Mkude, alieleza kuwa upande wa mashtaka tayari umewasilisha mashahidi watatu, ambapo shahidi wa mwisho alimaliza kutoa ushahidi wake jana Oktoba 23,2025.Hata hivyo, baada ya ushahidi huo kuwasilishwa, kulijitokeza pingamizi dhidi ya vielelezo vilivyotolewa.

“Upande wa mashtaka tulikuwa na mashahidi wengine waliotarajiwa kufuatia, lakini kwa sasa hatutawatumia kutokana na vielelezo kukataliwa.Tunaomba shauri hili liahirishwe hadi tarehe 3 Novemba 2025 kwa mujibu wa kifungu cha 302 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), kwani kwa leo hatuna shahidi,” alisema Wakili Issa.

Hoja za Utetezi

Katika kujibu ombi hilo, mshitakiwa Tundu Lissu alipinga hoja ya upande wa mashtaka akidai kuwa sababu zilizotolewa hazina msingi wa kisheria na kwamba kuahirisha kesi hiyo kunalenga tu kuchelewesha mwenendo wa shauri hilo.

“Waheshimiwa Majaji, sababu iliyotolewa ya kuomba ahirisho si ya msingi. Kesi hii yote inategemea vielelezo vilivyokataliwa na Mahakama Kuu. Hakuna shtaka lolote lililo nje ya vile vielelezo vilivyomo kwenye flash disk na memory card.Mashahidi waliobaki ushahidi wao unatokana na yaliyokuwa mtandaoni,” alisema Lissu.

Lissu aliongeza kuwa kuahirishwa kwa kesi hiyo kunalenga kumweka gerezani kwa muda mrefu zaidi hadi kipindi cha uchaguzi kimalizike, akisisitiza kuwa hana sababu ya kukimbia kesi.

“Leo ni siku ya 202 nikiwa gerezani ni zaidi ya miezi sita na nusu. Ombi la kuahirishwa likataliwe, na kama mtaahirisha, basi naomba dhamana kwa mujibu wa kifungu cha 302(2) cha CPA. Mimi sijawahi kukimbia kesi yoyote,” alisisitiza.

-Jamhuri Wakataa –

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Renatus Mkude alisisitiza kuwa ombi la kuahirisha shauri hilo linafuata misingi ya kisheria, akibainisha kuwa Jamhuri bado inaendelea na maandalizi ya ushahidi wake.

“Ni kweli tumetaja kifungu cha 302 kwa kuwa kwa sasa hatuna shahidi. Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 59(B), ufunguaji wa mashtaka unazingatia misingi ya haki. Masuala ya uchaguzi hayahusiani na kesi hii,” alisema Mkude.

Aliongeza kuwa hoja ya Lissu kudai kuwa hakuna kesi ni kuingilia majukumu ya upande wa mashtaka, na kwamba shtaka analokabiliwa nalo ni kati ya yale yasiyoruhusu dhamana.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Wakili wa Serikali Nassoro Katuga, aliyesema kuwa ombi la Lissu la kutaka kesi iendelee haliwezi kutekelezeka kwa sasa kutokana na ukosefu wa shahidi.

“Kifungu cha 302 kinaeleza wazi kuwa iwapo shahidi hayupo, basi ni busara ya mahakama kutumia mamlaka yake kuahirisha kesi,” alisema Katuga.

-Uamuzi wa Mahakama-

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, jopo la majaji lilitupilia mbali ombi la dhamana lililotolewa na Lissu na kukubaliana na ombi la upande wa mashtaka la kuahirisha shauri hilo.

“Mahakama imezingatia kuwa tangu kesi hii ianze, haijawahi kukosa shahidi. Hivyo, suala la kuahirisha shauri linafuata utaratibu. Kuhusu ombi la dhamana, kwa kuwa shtaka hili halina dhamana kisheria, mahakama haiwezi kutoa uamuzi huo,” amesema Jaji Ndunguru ambaye ametoa uamuzi huo kwa niaba ya jopo hilo.

Kwa msingi huo, shauli hilo limeahirishwa hadi tarehe 3 Novemba 2025, saa tatu asubuhi ambapo hii pia imetokana na mpangilio wa ratiba ya Mahakama ambayo ilitolewa wakati shauri hili linaanza katika Mahakama Kuu.

Lissu ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA na Mwanasiasa mashuhuri nchini Tanzania anakabiliwa na shtaka la Uhaini ambalo kwa mujibu wa Sheria za Tanzania ukipatikana na hatia adhabu yake ni kifo.

Kosa hilo anadaiwa kulitenda kutokana hotuba aliyoitoa Aprili 3,2025 akiwa wilaya ya Kinondoni ofisi za Chadema, kupitia mkutano na Waandishi wa habari.