Tundu Lissu Alalamikia Kutengwa na Udhalilishaji Gerezani

Kiongozi wa upinzani na Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ametoa taarifa kutoka gerezani akidai kutengwa na kudhalilishwa katika mazingira ya kizuizini.

Lissu Atoa Malalamishi ya Kutengwa gerezani na kudhalilishwa

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye akaunti yake ya X mnamo Oktoba 26, Lissu alisema kuwa chumba chake cha gereza kimefungwa kamera za CCTV zinazorekodi kila hatua yake, hata anapojisaidia au kubadilisha nguo.

“Chumba changu sasa kimefungwa kamera za ulinzi (CCTV) zinazorekodi kila ninachofanya, hata ninapojisaidia au kubadilisha nguo. Sina faragha tena kabisa. Hili si suala la usalama; ni kitendo cha makusudi cha kudhalilisha utu wangu,” alisema Lissu katika taarifa yake.

Kwa mujibu wa Lissu, wafungwa wenzake waliokuwa wakishiriki naye chumba hicho wameondolewa, na kumwacha peke yake bila mawasiliano ya kibinadamu.

Alieleza kuwa hali hiyo si ya kiusalama bali ni jaribio la makusudi la kudhalilisha utu wake, akitaja ukiukaji wa Kanuni za Mandela za Umoja wa Mataifa pamoja na Ibara ya 12 na 13 za Katiba ya Tanzania.

Lissu amekuwa rumande kwa zaidi ya siku 200 kwa tuhuma za uhaini, huku kesi yake ikisubiriwa kusikilizwa tena Novemba 3, siku chache baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.

Taarifa yake imeibuka wakati wa ongezeko la malalamiko kuhusu utekaji na kupotea kwa wanaharakati wa upinzani nchini Tanzania.

Haya yanajiri huku Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuhitimisha kampeni yake hii leo