Mwabukusi: Kumtuhumu Heche Kwa Ugaidi Ni Kuitia Aibu Taaluma Ya Sheria

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, ametoa kauli kali akilaani kile alichokiita matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa sheria unaofanywa na vyombo vya dola, hasa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (DPP) na Jeshi la Polisi.

Mwabukusi: Kumtuhumu Heche Kwa Ugaidi Ni Kuitia Aibu Taaluma Ya Sheria

Kupitia ujumbe aliouchapisha katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Mwabukusi alisema vyombo hivyo “vinamwaga petroli wakidhani wanazima moto,” akimaanisha kwamba matendo yao yanachochea zaidi sintofahamu badala ya kuimarisha usalama.

Mwabukusi alionyesha kukerwa na hatua ya kumhusisha mwanasiasa John Heche na tuhuma za ugaidi, akisema ni “udanganyifu wa kisheria” na “upuuzi unaoiaibisha taaluma ya sheria.” Aliandika: “It is an illusion kumtuhumu John Heche kwa ugaidi. Achaneni na huo upuuzi. Hali ya usalama siyo nzuri kuendelea na desturi zenu za kupika kesi ili kubambika watu. Mnatia aibu taaluma na mnakera.”

Kiongozi huyo wa TLS alidai kuwa Heche alikamatwa na kuzuiliwa kinyume cha sheria, na kwamba wakati wa tukio hilo, vyombo vya dola vilikuwa. “vikipanga mauaji ya raia huku vikimuweka mahabusu kinyume cha sheria.” Mwabukusi alisema ni wakati sasa kwa Mahakama “kukataa kutumika kama kokoro la kutekeleza uhalifu dhidi ya demokrasia,” akionya kwamba polisi na waendesha mashtaka wanapaswa kudhibitiwa kwa kuwa “wanataka kulipua moto ambao hautazimika.”

Rais huyo wa TLS alibainisha kuwa chama hicho kinachunguza kwa karibu matukio ya ukiukwaji wa haki unaodaiwa kufanywa na vyombo vya dola, akisema: “Sisi tunafuatilia habari hizi kwa ukaribu na tunaweka rekodi ya kila uhalifu mnaoufanya. Baadaye msije mkasema hatukuwaambia, kwa sababu hatutatumia hizi mahakama mlizozoea. Tutakwenda kule ambako tunajua aina hii ya makosa mnaoyatenda yanaweza kushughulikiwa.”

Mwabukusi alisisitiza kuwa TLS itatoa msaada wa kisheria kwa John Heche na familia nyingine zilizoathiriwa na vitendo vya ukatili au dhuluma, akisema chama hicho “kimesimama upande wa raia na katiba.” Aliongeza kuwa: “TLS itatoa msaada wa kisheria kwa John Heche dhidi ya dhuluma hii, na tutajitahidi kusaidiana na familia zote ambazo zimeathiriwa na ukatili wa polisi na jeshi dhidi ya maisha ya vijana wasio na hatia.”

Katika hitimisho lake, Mwabukusi aliwataka viongozi wa vyombo vya dola kutumia hekima na busara badala ya kutumia nguvu, akisisitiza kuwa vijana wa kizazi cha sasa ni wenye akili timamu na uvumilivu mkubwa. “Tuliwaonya kwa sauti, tukawafuata kwa unyenyekevu mkubwa na kuwaambia hawa vijana wa sasa siyo wale ambao hatuku reason. Nilisema hala hala kidole na jicho.

Kimsingi tumeaibika na mmeona kuwa risasi siyo kila kitu. Acheni vijana hawa wametulia kidogo kwa sababu wana busara kuliko sisi. Tusiwachokoze.”

Kauli ya Mwabukusi imeibua mjadala mpana katika medani ya sheria na siasa nchini, ambapo wadau mbalimbali wanasema ujumbe huo ni kumbusho muhimu kwa taasisi za dola kuhusu wajibu wao wa kikatiba kulinda haki, kuheshimu utu wa mwanadamu na kuzingatia misingi ya utawala wa sheria badala ya kutumia mamlaka kinyume cha sheria.