Kesi ya Uhaini Dhidi ya Tundu Lissu Yaahirshwa Kwa Sababu za Kiusalama

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imeahirishwa leo baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama kwamba mshtakiwa ameshindwa kufikishwa mahakamani kutokana na sababu za kiusalama.

Kesi ya Uhaini Dhidi ya Tundu Lissu Yaahirshwa Kwa Sababu za Kiusalama

Wakili wa Serikali, Thawabu Issa, akiwasilisha maelezo kwa niaba ya wenzake, alieleza kuwa baada ya kufika mahakamani na kutomuona mshtakiwa, walifanya mawasiliano na Jeshi la Magereza ambapo Mkuu wa Magereza aliwataarifu kwamba Lissu hakuweza kufikishwa mahakamani kwa sababu za kiusalama.

“Waheshimiwa majaji, mshtakiwa Tundu Lissu hayupo mahakamani, na tumejulishwa na Mkuu wa Magereza kwamba ameshindwa kumleta kutokana na sababu za kiusalama,” alisema Wakili Issa.

Awali, shauri hilo lilipangwa kuendelea Oktoba 3, 2025, lakini halikufanyika kutokana na changamoto za kiusalama zilizokuwapo wakati huo. Leo, kesi hiyo ilikuwa imepangwa kuendelea kwa shahidi wa nne wa upande wa mashtakakutoa ushahidi, baada ya shahidi wa tatu, ambaye ni mtaalamu wa video, kumaliza kutoa ushahidi wake.

Aidha, Wakili Issa aliomba Mahakama iahirishe shauri hilo kwa siku 14, akieleza kuwa hata mashahidi waliopangwa kufika kutoka mikoa ya Ruvuma na Mbeya wameshindwa kufika kutokana na hali hiyo ya kiusalama.

“Kwa muktadha huo, Waheshimiwa majaji, tumeshindwa kuwapata mashahidi leo kwa ajili ya kuendelea na usikilizaji. Tunaomba shauri liahirishwe chini ya kifungu cha 302(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, kama ilivyorekebishwa mwaka 2023,” alisema.

“Tunaomba Mahakama itupatie siku 14 ili hali ya kiusalama iwe imetengamaa na tuweze kuendelea na shauri,” aliongeza.

Baada ya kusikiliza maombi hayo, jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru liliagiza kuwa kesi hiyo iendelee Jumatano, Novemba 12, 2025, na kuwataka upande wa mashtaka kuhakikisha mashahidi wanapatikana siku hiyo.

Aidha, Jaji Ndunguru aliliagiza Jeshi la Magereza kumfikisha mshtakiwa mahakamani siku hiyo kwa ajili ya kuendelea na usikilizaji wa kesi.