Mapigano kati ya serikali ya Ethiopia na kikosi cha jeshi kutoka eneo la kaskazini la Tigray yamesababisha mzozo wa kisiasa nchini Ethiopia. Mapigano yamekuwa yakiendelea tangu Novemba 2020 na kusababisha njaa kali na vifo vya takriban watu 400,000 kufikia sasa.
Mgogoro, kung’ang’ania madaraka, uchaguzi na msukumo wa mageuzi ya kisiasa ni miongoni mwa mambo yanayochangia machafuko Ethiopia.
Ubalozi wa Amerika mjini Addis Ababa umewashauri raia wake na wanadiplomasia kuondoka.
Wakati huo huo, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametoa wito kutaka hatua za haraka kuchukuliwa kuzuia ghasia kwa kuwa athari zake zinaweza kuhatahatarisha usalama wa kanda ya Afrika Mashariki.
Historia ya siasa na uongozi Ethiopia
Nchi ya Ethiopia, rasmi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, ni nchi ya takriban watu 117 milioni. Fasihi simulizi inaeleza kuwa utawala wa kifalme ulianzishwa na nasaba ya Solomoni kutoka kwa Mfalme Sulemani na Malkia wa Sheba chini ya mfalme wa kwanza Menelik wa kwanza.
Katika karne ya 20, Ethiopia ilikuwa taifa pekee la Kiafrika lililofanikiwa kujilinda dhidi ya ukoloni wa Ulaya, na kuishinda Italy katika vita vya Adwa. Kufuatia mapungufu ya uongozi wa kifalme pamoja na migogoro na misukosuko ya ndani, Mtawala Haile Selassie alipinduliwa mwaka wa 1974 na uongozi wa Kifalme ukakomeshwa.
Jeshi la Derg lilichukua uongozi wa nchi na kwa miaka 16, kundi la Derg na kundi la waasi kutoka Tigray na Eritrea waliongoza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 16. Mwaka wa 1987 iliunda serikali ya People’s Democratic Republic of Ethiopia iliyopinduliwa mwaka wa 1991 na Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front (EPRDF).
Serikali ya muungano kati ya EPRDF na vyama vingine vitatu vya kisiasa na iliyotawaliwa na kundi la TPLF ilileta mabadiliko na kuundwa kwa serikali ya shirikisho iliyojumuisha majimbo 10 ya Ethiopia.
Serikali ya muungano chini ya EPRDF ilikomeshwa mara tu Abiy Ahmed alipokuja uongozini mwaka wa 2018 kama Waziri mkuu, aliunganisha vyama tofauti vya kisiasa Ethiopia na kuunda chama cha Prosperity Party mwaka wa 2019.
Ingawa serikali ya Abiy hapo awali ilirekebisha na kukomboa siasa za nchi kulikuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu, hasa machafuko ya kikabila na uhasama kati ya serikali ya Abiy na wanachama wa TPLF yaliyochangia machafuko na mapigano katika jimbo la Tigray yaliyoanza Novemba 2020.
Chimbuko la mapigano Tigray
Mzozo katika jimbo la kaskazini la Tigray ulianza tarehe 4 Novemba wakati Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliamuru mashambulizi ya kijeshi dhidi ya vikosi vya Tigray. Ahmed alisema alichukua hatua hiyo baada ya jeshi la TPLF kushambulia kambi ya wanajeshi wa serikali ya shirikisho.
Mapigano yalichangiwa zaidi na uhasama kati ya serikali ya Abiy na viongozi wa chama cha Tigray.Kwa miongo mitatu, muungano wa chama cha TPLF na EPRDF ulikuwa uongozini, baada ya Abiy Ahmed kuingia madarakani jimbo la Tigray lilihisi kutengwa na serikali kuu. Abiy alipojaribu kuunganisha vyama vyote vya kisiasa chini ya muungano mmoja wa Prosperity Party,Tigray ilipinga na mzozo wa kisiasa ukazuka.Viongozi wa Tigray waliona mageuzi yaliyopendekezwa na Abiy kama jaribio la kuharibu mfumo wa shirikisho la Ethiopia.
Uhasama kati ya Tigray na serikali kuu ulichangiwa na uamuzi wa Tigray kufanya uchaguzi katika jimbo lake huku serikali kuu ikiwa imeahirisha uchaguzi huo katika majimbo mengine kutokana na kuwepo kwa janga la UVIKO 19.
Madai ya kuwa jeshi la TPLF liliiba silaha kutoka kambi ya kijeshi ya shirikisho yalimfanya Abiy kutangaza vita dhidi ya TPLF na jimbo la Tigray.
Majeshi ya TPLF yameendeleza vita na kuiteka miji ya Amhara na Afar na wanaelekea mji mkuu wa Addis Ababa.