Marekani imeondoa majeshi yake Afghanistan, na kumaliza vita vya muda mrefu katika historia ya taifa hilo. Wataliban nao kwa upande wao wamesheherekea kwa kupiga risasi hewani katika mji mkuu wa Kabul,hatimaye wamepata uhuru wao.
Wapiganaji wa Taliban walifanikiwa kuchukuka utawala wa Afghanistan baada ya kuiteka miji tofauti nchini humo bila upinzani wowote. Rais wa Afghanistan, Ashraf Ghani akikimbilia Falme za Kiarabu siku moja kabla yawapiganaji wa Taliban kuchukua udhibiti wa Mji Mkuu, Kabul.
Wanajeshi wa mwisho wa Marekani waliokuwa wakisimamia uokoaji wa wakimbizi wa mwisho kutoka uwanja wa ndege wa Kabul wameondoka Jumatatu usiku,huku kukiibuka maswali kuhusu nguvu ya taifa la Marekani.
Ndege hiyo ya mwisho ya Jeshi la Marekani, aina ya Boeing C-17 imeondoka huku kati ya Wamarekani 100 hadi 200 wakiwa bado nchini humo, pamoja na maelfu wengine waliosaidia utawala wa Marekani nchini humo kwa miaka 20 iliyopita
Mara tu ndege ya Marekani ilipopaa angani, wanamgambo wa Taliban walimiminika katika uwanja wa ndege na kusheherekea ushindi wao miaka 20 baada ya Marekani kuwaondoa madarakani.Wanajeshi wa mwisho wameondoka nchini humo kabla siku ya mwisho ya 31 Agosti iliyokuwa imewekwa na Rais wa Marekani Joe Biden.
Vita hivyo vya zaidi ya miaka 20 vikiwa vimesababisha vifo vya takriban wanajeshi 2,400 wa Marekani na vifo vya maelfu ya raia wa Afghanistan,kama shambulizi la hivi maajuzi la Marekani katika uwanja wa ndege wa Kabul lililowauwa watu 10 wa familia moja ikiwemo baba na watoto wake wanne.
Zaidi ya watu 123,000 wamehamishwa kutoka Kabul katika shughuli ya uokoaji iliyoanza Agosti 14.Rais wa Marekani, Joe Biden amesema atahutubia taifa Jumanne mjini Washington Marekani.