Lissu Aelezea Dhulma Anayodai Kufanyiwa Na Maafisa Wa Magereza

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, ameeleza malalamiko yake kuhusu kile alichodai kuwa ni dhulma na ukiukwaji wa haki zake za msingi unaofanywa na maafisa wa Magereza ya Ukonga tangu kesi yake ilipoahirishwa Novemba 12, 2025.

Lissu Aelezea Dhulma Anayodai Kufanyiwa Na Maafisa Wa Magereza

Akizungumza mahakamani, Lissu alianza kwa kuwatakia waheshimiwa majaji heri ya mwaka mpya, kisha akaeleza kuwa ana masuala matatu ya msingi aliyohitaji kuyaweka kwenye kumbukumbu rasmi za Mahakama.

Lissu alisema masuala mawili kati ya hayo yanawahusu moja kwa moja waheshimiwa majaji kwa kuwa ni miongoni mwa viongozi wanaotembelea magereza, na hivyo wana wajibu wa kuhakikisha haki za wafungwa na mahabusu zinalindwa. Alisisitiza kuwa wafungwa wana haki ya kutoa malalamiko yao kwa majaji wanaotembelea magereza kuhusu mazingira na namna wanavyotendewa.

Katika hoja yake ya kwanza, Lissu alieleza kuwa haki yake ya kuwasiliana na mawakili wake imekuwa ikikiukwa kwa muda mrefu, akidai kuwa maafisa wa magereza wamekuwa wakisikiliza mazungumzo yake na mawakili wake kinyume na sheria.

Alifafanua kuwa tukio hilo lilianza awali katika Mahakama ya  Kisutu wakati wa usikilizwaji wa awali wa kesi yake na kushughulikiwa, lakini limejitokeza tena tangu kesi yake ilipoahirishwa Novemba 12, 2025.

Kwa mujibu wa Lissu, tangu siku hiyo mawakili wake wanapofika gerezani, maafisa wa magereza wamekuwa wakimzingira na kusikiliza mazungumzo yao.

Alidai kuwa kwa siku 88 mfululizo hakuweza kuzungumza kwa uhuru na mawakili wake, huku akiambiwa kuwa hali hiyo inatokana na maagizo kutoka ngazi za juu.

Hoja ya pili aliyoiwasilisha mahakamani inahusu kuzuiwa kutembelewa na ndugu, jamaa na viongozi. Lissu alisema kuwa tangu alipowekwa mahabusu Aprili 10, 2025 hadi kesi ilipoahirishwa Novemba 12, 2025, alikuwa akitembelewa bila tatizo.

Hata hivyo, baada ya tarehe hiyo, alidai kuwa aliitwa na mkuu wa gereza na kuambiwa kuwa viongozi pamoja na ndugu hawaruhusiwi tena kumtembelea.

Katika hoja ya tatu, Lissu alielezea wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa kesi yake, akisisitiza kuwa hamlaumu waheshimiwa majaji wala mawakili wa Serikali.

Alidai kuwa haki zake zimekiukwa kutokana na kucheleweshwa kwa kesi hiyo kwa muda mrefu.

Alieleza kuwa amekuwa mahabusu kwa siku 307, sawa na miezi kumi, huku kesi hiyo ikisikilizwa kwa siku 15 tu tangu kuanza kwake.

Alisisitiza kuwa haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa, akirejea matakwa ya Katiba inayozitaka Mahakama kuendesha mashauri kwa wakati bila kuchelewesha haki.

Lissu aliongeza kuwa utaratibu wa kuendesha kesi kwa mfumo wa “session” umechangia kwa kiasi kikubwa kucheleweshwa kwa kesi yake, akidai kuwa mfumo huo haukidhi mahitaji ya kesi nzito kama ya uhaini, ambayo kwa mujibu wake ni kosa la kipekee linalohitaji usikilizwaji wa haraka na wa makini.

Aliwaonya waheshimiwa majaji kuwa kuna hatari kubwa ya kesi hiyo kuendelea kucheleweshwa endapo utaratibu huo utaendelea kutumika bila kufanyiwa marekebisho.