Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imeahirishwa hadi Februari 11, 2026, ambapo jopo la majaji watatu linatarajiwa kutoa uamuzi mdogo kuhusu hoja za mapingamizi zilizowasilishwa na mshtakiwa dhidi ya upande wa mashtaka.

Katika usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa Jamhuri uliwasilisha hoja zake mahakamani kujibu mapingamizi ya mshtakiwa, ukisisitiza kuwa hatua zilizochukuliwa na Mahakama kuhusu ushahidi wa mashahidi ziko ndani ya misingi ya kisheria.
Wakili wa Serikali Mkuu Nasoro Katuga alisema kuwa moja ya hoja kuu zilizojadiliwa inamhusu shahidi wa upande wa mashtaka anayejulikana kwa jina la kificho P11, ambaye alifika mahakamani kuendelea na ushahidi wake.
Katuga alieleza kuwa mshtakiwa alipinga shahidi huyo kuendelea kutoa ushahidi kwa madai kuwa kizimba maalumu kilichopo mahakamani hapo si kizimba halali cha mashahidi kwa mujibu wa tafsiri ya kanuni husika. Kwa mujibu wa mshtakiwa, mpangilio wa kizimba hicho haukumwezesha yeye wala Mahakama kumuona shahidi wakati wa utoaji wa ushahidi.
Hata hivyo, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa shahidi P11 yuko chini ya ulinzi maalumu uliotolewa kwa amri ya Mahakama, na kwamba hatua hizo zililenga kulinda usalama wake.
Katuga alisisitiza kuwa hoja ya mshtakiwa ya kudai kutomuona shahidi haiwezi kusimama kisheria kutokana na mazingira ya ulinzi yaliyopo.
Akiendelea kufafanua, Wakili Katuga aliirejea hoja ya tano ya mshtakiwa, ambayo ilijikita kwenye Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi zilizoanza kutumika rasmi Julai 11, 2025.
Alinukuu Kanuni ya 6 ya kanuni hizo, akibainisha kuwa Mahakama ina mamlaka ya kutoa maelekezo na kuamuru hatua mbalimbali za ulinzi kwa mashahidi inapobaini ulazima wa kufanya hivyo.
Kwa upande wake, mshtakiwa Tundu Lissu aliwasilisha hoja zake, akisisitiza kuwa kizimba kilichotumika hakiwezi kutambuliwa kama kizimba cha mashahidi kwa mujibu wa kanuni na tafsiri ya kisheria. Alidai kuwa kizimba hicho hakionekani na waheshimiwa majaji, hali ambayo kwa mtazamo wake inakiuka misingi ya usikilizwaji wa haki.
Lissu pia alihoji iwapo amri ya Mahakama ya kutoa ulinzi kwa shahidi ilijumuisha moja kwa moja matumizi ya kizimba hicho maalumu, akieleza kuwa upande wa mashtaka haukuomba kwa uwazi ulinzi wa mashahidi wao kupitia matumizi ya kizimba cha mashahidi.
Aidha, alieleza kuwa awali upande wa mashtaka uliwasilisha hoja kuwa mashahidi hao hawajulikani na mtu mwingine yeyote isipokuwa waendesha mashtaka au maafisa wa polisi waliowachukua maelezo yao.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Februari 11, 2026 kwa ajili ya kutoa uamuzi mdogo kuhusu mapingamizi hayo.