Shahidi wa Siri P5 Asimulia Video ya Lissu Ilivyompa Hofu

Shahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu ameeleza jinsi video aliyodai kuiona mtandaoni ilivyomwingiza kwenye hofu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Shahidi wa Siri P5 Asimulia Video ya Lissu Ilivyompa Hofu

Shahidi huyo, mwenye umri wa miaka 33 na mkazi wa Kibangu, wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam, aliiambia Mahakama kuwa anajishughulisha na biashara ndogondogo ya kuuza viatu na soksi katika maeneo ya Mchikichini, Feri na Posta Mpya. Pia hufanya kazi ya kuosha magari mara kwa mara.

 

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Ajuaye Nzegeri, shahidi huyo wa siri P5 akiwa kwenye kizimba cha siri, alidai kuwa Aprili 4, 2025, akiwa eneo la Posta Mpya karibu na benki ya NBC alipokua amejipumzisha aliona video kupitia mtandao wa Facebook akitumia simu yake ya mkononi. Kwa mujibu wake, video hiyo ilimuonesha Tundu Lissu akiwa jukwaani, amevaa gwanda la kaki na fulana nyeusi, huku nyuma kukiwa na bendera ya Taifa.

 

Wakili Ajuaye Nzegeri:Shahidi unaishi wapi?

Shahidi:Naishi Kibangu wilaya ya ubungo Dar es Salaam.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Unafanya kazi gani?

Shahidi:Nafanya kazi ya Machinga na saa nyingine naosha magari

Wakili Ajuaye Nzegeri:Katika kazi yako ya umachinga unauza bidhaa gani?

Shahidi:Viatu saa ingine soksi.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Unafanyia shughuli zako maeneo gani?

Shahidi:Nafanyia maeneo ya Mchikichini, Posta Mpya hadi Feri.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Elezwa Mahakama  April 4, 2025 ulikuawapi?

Shahidi:Nilikua Posta mpya maeneo “Garden” karibu na benki ya NBC, nimejipumzisha huku nikiperuzi kwenye simu yangu.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Eleza ulikua unaperuzi kwenye mitandao gani

Shahidi:Facebook, WhatsApp na You Tube.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Ulikua unaperuzi kwa kutumia nini?

Shahidi:Simu ya Smartphone aina Sony Xperier Galaxy.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Wakati sasa unaperuzi hiyo mitandao ya kijamii uliona nini?

Shahidi:Baada ya kuangalia niliona video ndogo ambayo ilikua ikimuonesha Tundu Lissu, kwenye mtandao wa Facebook.

Wakili Ajuaye Nzegeri: Shahidi unawezaje kuingia kwenye mtandao wa Facebook.

Shahidi:Ni lazima uwe na account halafu lazima simu iwe na bando la kutosha. Mimi nilikua tayari nina “account” yangu.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Shahidi huyo

Tundu Lissu Unamfahamu.

Shahidi:Namfahamu kwa kumuona na kupitia mitandaoni.

Wakili Ajuaye Nzegeri: Huyo Tundu Lissu ni nani?

Shahidi:Tundu Lissu ni mwanasiasa.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Sasa Shahidi tuambie baada ya kuona hiyo video ullifanya nini?

Shahidi:Baada ya kuona hiyo video nilifungua nikitaka kujua anasema nini?

Wakili Ajuaye Nzegeri:Sasa baada ya kuzicheza ukashuhudia kitu gani?

Shahidi:Nilimsikia akisema atahakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 hautafanyika atahakikisha atakinukisha.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Uchaguzi wa kutu gani?

Shahidi:Uchaguzi ulikua unahusu Wabunge, Madiwani pamoja na Rais

Wakili Ajuaye Nzegeri:Shahidi kitu gani kingine ulikisikia kwenye video ile?

Shahidi:Nilimsikia akisema polisi wanaiba kura na pia nilimsikia akisema majaji nao ni MaCCM hawatendi haki.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Shahidi hiyo video uliyoiona ulimuona akiwa wapi

Shahidi:video niliyomuona alikua jukwaani.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Ulimuona akiwa na muonekano gani?

Shahidi:Nilimuona akiwa amevaa gwanda la kaki ndani akiwa amevaa T- shirt nyeusi nyuma kulikua na bendera ya Taifa.

Shahidi aliiambia Mahakama kuwa katika video hiyo alimsikia Lissu akisema atahakikisha uchaguzi mkuu wa 2025 haufanyiki na kwamba “atahakikisha wanakinukisha.” Aidha, alidai kumsikia akisema polisi wanaiba kura na kwamba majaji ni wanachama wa CCM wasiotoa haki.

Baada ya kuitazama video hiyo, shahidi alisema alirejea nyumbani Ubungo na kupita katika kijiwe cha kahawa, ambako alikuta mjadala mkali kuhusu kauli hizo. Alidai kuwa baadhi ya waliokuwepo walionesha kuunga mkono kauli hizo, jambo lililoongeza hofu yake kuhusu uwezekano wa vurugu siku ya uchaguzi.

Kutokana na hofu hiyo, shahidi alisema alimtafuta ndugu yake kwa simu, ambaye alimtambulisha kama askari polisi anayefanya kazi Tabata Relini, ili kupata ufafanuzi. Alidai ndugu yake alimweleza kuwa vyombo vya usalama vinafahamu suala hilo na vinaendelea kulifuatilia.

Shahidi:Baada ya kuona hiyo video niliondoka kuelekea kituo cha daladala na kurudi nyumbani ubungo.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Elezea baada ya kushuka kituo cha dalala ulielekea wapi

Shahidi:Nilishukua kituo cha daladala nikaelekea maskani kijiwe cha kahawa

Wakili Ajuaye Nzegeri:Elezea mahakama hii sasa baada ya kufika kijiweni ulikuta nini?

Shahidi:Nilikuta mzozo kila mmoja akiwa na hoja zake kuhusiana na video ile.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Huo mzozo ulikuaje?

Shahidi:Wengi walikua wanaunga mkono kauli yake wakisema watahakikisha watakinukisha siku ya kupiga kura.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Hapo kijiweni uliona nini kingine?

Shahidi:Baada ya hapo kupitia mzozo ule niliona kutakua na fujo siku ya uchaguzi.

Shahidi:Niliona kupitia mzozo ule niliona amani itavurugika kwa sisi tunaotafuta kupita mitaani na kupata njaa.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Shahidi baada ya kushuhudia kiliendelea nini kingine.

Shahidi:Nilitoka kwenda nyumbani.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Ulifanya nini?

Shahidi:Niliingiwa na uwoga nikampigia ndugu yangu simu kumueleza umeyaona ya huku mtandaoni kuhusiana na Lissu?

Wakili Ajuaye Nzegeri:Huyo ndugu yako uliyempigia anafanya kazi gani

Shahidi:Yeye ni Askari Polisi.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Shahidi ni Polisi wapi.

Shahidi:Yeye ni Polisi Tabata Relini.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Sasa eleza baada ya kumpigia huyo ndugu yako alikujibu nini?

Shahidi:Alinijibu kuwa tumelisikia na tunalifatilia kikamilifu na alinitaka nisiwe na wasiwasi kuhusu suala hilo.

Wakili Ajuaye Nzegeri:Ni kitu gani kilikufanya mpaka uingie na hofu.

Shahidi:Nilipata hofu na lile neno tutakinukisha kwa sababu kutakua na uvunjifu wa amani.

Shahidi aliendelea kueleza kuwa Aprili 9, 2025 alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kama askari, akimtaka afike Kituo cha Polisi Central kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na video hiyo. Alisema alifika kituoni, akaandika maelezo na baadaye kuruhusiwa kuondoka.

Aidha katika ushahidi wake shahidi huyo alisema hofu yake iliyotokana na maneno aliyoyazungumza Lissu kupitia video aliyoiona ndio kilichotokea Oktoba 29 siku ya uchaguzi

Hata hivyo, wakati wa maswali ya dodoso kutoka upande wa utetezi, Lissu alipinga baadhi ya maelezo ya shahidi, akionesha kuwa mambo kadhaa aliyoyataja mahakamani hayakuwepo katika maelezo yake ya awali kwa polisi.

Miongoni mwa mambo hayo ni aina ya simu aliyotumia, mitandao aliyotembelea, mavazi aliyodai kumuona nayo mshtakiwa, pamoja na maelezo kuhusu mjadala wa kijiweni na mawasiliano na ndugu yake askari.

Lissu:Umesema katika ushahidi wako kwamba wewe unafanya kazi ya umachinga kweli si kweli?

Shahidi: Ndio nafanya?

Lissu:Una leseni ya biashara?

Shahidi: Sina ila najiandaa?

Lissu: Una kitambulisho cha Nida?

Shahidi: Kitambulisho sina ila nitakipata

Lissu: Una kitu chochote kinachokufanya uoenekane wewe ni Mfanyabiashara?

Shahidi:Kitu chochote ni biashara ninayoifanya

Lissu: Watajuaje kama hujaleta bidhaa hapa?

Shahidi:Wataniamini kwa sababu nafanya biashara.

Lissu:Umesema unakaa Ubungo Kibangu.

Shahidi: Kweli

Lissu:: Nyumba yako au umepanga?

Shahidi: Nimepanga

Shahidi pia alikiri kuwa hakuiwasilisha mahakamani video aliyodai kuiona, wala hakufahamu akaunti ya Facebook iliyochapisha video hiyo.

Akijibu swali kuhusu maana ya neno “kukinukisha,” shahidi alisema kwa uelewa wake linaashiria kuchochea fujo au vurugu. Aliongeza kuwa siku ya uchaguzi alikaa ndani kwa siku sita kwa hofu, hali iliyomfanya kukosa kipato.

Shahidi huyo amemaliza kutoa ushahidi wake huku ikitazamiwa kuendelea kwa shahidi mwingine kabla ya kesi kuahirishwa.

Itakumbukwa kuwa Lissu anakabiliwa na mashtaka ya Uhaini ambayo kwa mujibu wa sheria za Tanzania hukumu yake ni kifo.