Shahidi wa tisa wa upande wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ametoa ushahidi wake leo mahakamani akieleza wasifu wake, tukio la kukamatwa kwa watuhumiwa wawili na hatua za uchunguzi alizochukua.

Shahidi huyo, PF 18544 ASP Geofrey Agrey (47), mkazi wa Arusha, aliiambia Mahakama kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi anaefanya kazi katika Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Arusha akiwa na uzoefu wa miaka 15 katika kazi ya upelelezi.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Renatus Mkude, mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru shahidi alisema alipata mafunzo ya awali katika Chuo cha Polisi Moshi, ikiwemo mafunzo ya upelelezi na ya “Nyota ya Kwanza” mwaka 2015. Aidha, alimaliza mafunzo ya cheo cha Mrakibu wa Polisi katika Chuo cha Polisi Dar es Salaam mwaka 2025.
Alieleza kuwa alianza kazi kama askari wa general duty katika kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam, baadaye akahamishiwa Geita katika Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, kabla ya kuhamia Arusha mwaka 2025.
Shahidi alidai kuwa Aprili 3, 2025 alikuwa katika doria jijini Arusha akiwa na askari wengine wanane, wakitumia gari aina ya Toyota. Wakiwa doria, alipokea maelekezo kupitia *radio call* kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, Boni Mgogo, kuhusu taarifa za vijana wanaodaiwa kuhamasishana kuzuia Uchaguzi Mkuu wa 2025 katika eneo la Mromboo
Alisema walifika katika kijiwe cha bajaji na kuwakuta vijana wawili wakijadili suala hilo. Aliwaweka chini ya ulinzi, lakini walijaribu kukimbia kabla ya kukamatwa. Watuhumiwa hao, waliotajwa kama P4 na P7, walipelekwa Kituo cha Polisi Murieti.
Shahidi alieleza kuwa wakati akiwapeleka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO), aliwahoji kuhusu madai ya kula njama za kuzuia uchaguzi. Kwa mujibu wake, watuhumiwa walidai wanaunga mkono kauli za Tundu Lissu za kuzuia uchaguzi.
Baadaye alifungua jalada la uchunguzi na kuandika maelezo yake tarehe 18 Aprili 2025.
Katika hatua ya kumhoji shahidi, Lissu alianza kwa kuhoji maadili na weledi wa Jeshi la Polisi, akimtaka shahidi athibitishe kama Polisi hufundishwa kuwa waongo au kuongeza maneno kwenye ushahidi. Shahidi alikanusha na kusisitiza kuwa Polisi hufundishwa maadili na weledi.
Lissu alirejea Police General Orders (PGO), akimtaka shahidi athibitishe kuwa PGO zinawataka askari kuwa waaminifu, wasio na upendeleo na wenye weledi, jambo ambalo shahidi alikubali.
Hata hivyo, Lissu alibainisha kuwa baadhi ya mambo aliyoyaeleza shahidi mahakamani ikiwemo uzoefu wake wa miaka 15, kushiriki doria akiwa na askari tisa, kupokea maelekezo kutoka kwa Mgogo na kuwahoji watuhumiwa njiani hayakuandikwa katika maelezo yake ya polisi.
Shahidi alikiri kuwa vipengele hivyo havikuwepo katika maelezo yake yaliyoandikwa.
Lissu alihoji ni kwa mujibu wa sheria gani kuzuia uchaguzi ni kosa la jinai, ambapo shahidi alijibu kuwa hawezi kujua.
Aidha, alihoji uhalali wa shahidi kujiandikia maelezo yake mwenyewe, kujionya na kujishuhudia, akitaka afafanue kama PGO au Kifungu cha 10(3)(d) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai vinamruhusu kufanya hivyo.
Katika baadhi ya maswali hayo, shahidi alisema “siwezi kujua” au alikaa kimya.
Baada ya utetezi kumaliza maswali, upande wa Jamhuri ulirejea kwa maswali ya kusawazisha, ambapo shahidi alisisitiza kuwa aliandika maelezo yake kama askari wa Polisi na ana mamlaka ya kufanya hivyo.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa mahakamani.