Shahidi Akiri Kutojua Sheria ya Inayoeleza Kuzuia Uchaguzi ni Kosa

Kauli ya “sifahamu sheria gani” kutoka kwa Shahidi wa 12 wa Jamhuri imeibua mshangao katika kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, inayoendelea katika Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Dar es Salaam.

Shahidi Akiri Kutojua Sheria ya Inayoeleza Kuzuia Uchaguzi ni Kosa

Shahidi huyo, H937 Detective Koplo Vicent Kipii (36), Askari Polisi wa Kituo cha Central Mbeya, ni shahidi wa 12 kati ya mashahidi 30 wa Jamhuri wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Ignac Mwinuka, shahidi alianza kwa kujitambulisha na mahali anakoishi.

Alieleza kuwa anaishi Mbeya Mjini, amejiunga na Jeshi la Polisi mwaka 2011 na kuhitimu mafunzo Machi 30, 2012 katika Chuo cha Polisi Moshi. Kwa sasa anafanya kazi Kituo cha Polisi Central Mbeya tangu 2022, na ana uzoefu wa miaka sita katika kitengo cha upelelezi.

Akieleza tukio la Aprili 4, 2025, alisema alipokuwa kituoni aliitwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mwanjelwa na kupewa jukumu la kumkamata mtu anayejulikana mahakamani kama P9.

Amedai kuwa baada ya kupewa maelezo hayo alipatiwa namba yake ili aweze kumfatilia, ambapo alimpigia kama alivyoelekezwa na kujifanya mteja anataka huduma ya umeme nyumbani kwake.

Alisema baada ya kumpigia walikubaliana kukutana eneo la Kabwe, Mbeya, ili waweze kwenda nyumbani kwa ajili ya huduma aliyoitaka.

Hata hivyo alipofika hapo sehemu ya makutano alimkuta P9, lakini mambo yakawa tofauti na alivyoelezwa kwenye simu kwani alimwambia kuwa hana shida na huduma aliyoiomba bali alitaka kumkamata kwa kosa la kuhamasisha vurugu  na kuzui uchaguzi.

“Nilipokutana naye nilijitambulisha kuwa mimi ni Askari Polisi na nikamweleza kuwa namkamata kwa kosa la uchochezi, kuhamasisha kuzuia uchaguzi wa 2025,” aliiambia Mahakama.

Kwa mujibu wa shahidi, mtuhumiwa hakutoa upinzani, na ndipo alipoongozana nae kwenda kituo cha polisi bila ubishi.

Bahati nzuri alikuwa muelewa, tukaongozana hadi Kituo cha Polisi Mwanjelwa nikamkabidhi”Katika hatua ya kumhoji maswali ya dodoso Lissu alianza kwa maswali ya utambulisho kabla ya kuelekeza nguvu kwenye taratibu za uandishi wa maelezo na msingi wa kisheria wa kosa lililotajwa.

Katika mahojiano hayo Lissu alitak kujua iwapo kuna mtu aliyeshuhudia wakati anaandika maelezo yake Polisi

Lissu: Kuna aliyeshuhudia wakati unaandika maelezo yako?

Shahidi: Niliandika mwenyewe, hakuna aliyeshuhudia.

Alikiri pia kuwa katika maelezo yake hakumtaja jina la Mkuu wa Kituo aliyempa maagizo ya kumkamata P9.

Mjadala mkubwa ulijitokeza pale Lissu alipomuuliza ni kwa sheria ipi kosa la kuzuia uchaguzi linatajwa, ambapo Shahidi alieleza kuwa hafahamu sheria gani isipokua anachojua kuzuia uchaguzi ni kosa.

Lissu: Kwa sheria ipi?

Shahidi: Sifahamu sheria gani.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa kwa ufahamu wake kuzuia uchaguzi ni kosa.Aidha, alipoulizwa kuhusu shtaka la Uhaini linalomkabili Lissu, shahidi alisema anafahamu Lissu anashtakiwa kwa Uhaini lakini alikiri hafahamu vipengele vyote vya shtaka hilo zaidi ya madai ya kauli zinazohusiana na uchaguzi.

Kesi inaendelea ambapo Shahidi wa 13 P3 anaendelea kutoa ushahidi wake.