Mvutano mkali wa kisheria umeibuka katika kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kufuatia hoja kuhusu uhalali wa taarifa “Notice” iliyowasilishwa na upande wa Jamhuri kuomba kuongezea maelezo ya ushahidi wa shahidi ACP Amini Maamba.

Shauri hilo lilipangwa kwa ajili ya wasilisho maalum kuhusiana na Notice hiyo, ambayo utetezi umeieleza kuwa si Notice halali kwa mujibu wa sheria za Tanzania.
Wakili Mkuu wa Serikali, Nassoro Katuga, aliiambia Mahakama kuwa Februari 18, 2026, upande wa Jamhuri uliwasilisha kwa njia ya mtandao Notice ya kuwasilisha ushahidi wa nyongeza chini ya Kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 20, Mapitio ya 2023.
Kwa mujibu wa Wakili Katuga, pamoja na Notice hiyo, waliwasilisha pia kiini ama msingi wa ushahidi “substance of evidence” kama inavyotakiwa na kifungu cha 308(2).
Alieleza kuwa ushahidi huo hauleti shahidi mpya bali unaongeza maelezo ya ushahidi wa shahidi aliyekwisha kutoa ushahidi wake, ACP Amini Maamba, ambaye alikuwa kiongozi wa timu ya upelelezi wa matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi.
Katuga alifafanua kuwa kifungu cha 308(4) kinaeleza wazi kuwa “substance of evidence” inajumuisha ushahidi uliopo kwenye nyaraka au rekodi, na kwamba ushahidi wanaotaka kuwasilisha ulikuwepo lakini haukusomwa wakati wa mwenendo wa shauri katika Mahakama ya Ukabidhi ya Kisutu.
Alidai kuwa mapungufu hayo yaligundulika Februari 16, 2026, wakati wa maandalizi ya ushahidi wa ACP Maamba, ndipo ikaonekana kuwa baadhi ya vipengele havikuwasilishwa kikamilifu wakati wa Committal.
Aidha, alisisitiza kuwa kifungu cha 308 hakijaeleza muundo maalum wa Notice, bali kinahitaji tu jina, anuani na substance ya ushahidi mambo ambayo, kwa mujibu wake, yamekidhiwa.
Katika msingi wa wasilisho lake Katuga ameiomba Mahakama ikubaliane na maombi ya Jamhuri na kutupilia mbali pingamizi la mshtakiwa.
Kwa upande wake, mshatakiwa Tundu Lissu ambaye anajitetea mwenyewe katika kesi hiyo, alipinga vikali hatua hiyo, akisema Notice hiyo haina msingi wa kisheria.
Lissu alisema kifungu cha 308(1) kinahusu shahidi mpya yaani shahidi ambaye maelezo yake hayakusomwa wakati wa Committal.
Lakini katika kesi hii, shahidi anayezungumziwa, ACP Amini Maamba, tayari alitajwa kama shahidi namba 26 na maelezo yake yalisomwa wakati wa Committal.
Aliitaka Mahakama kurejea rekodi ya ukurasa wa 134 wa Mahakama ya Ukabidhi, akieleza kuwa mlango wa ushahidi wa shahidi huyo tayari ulifungwa kisheria.
“Sasa maelezo ya shahidi ambaye tayari maelezo yake yalisomwa yanaingizwa vipi tena kupitia Notice inayodai kuwasilisha nyongeza?” alihoji.
Kwa mujibu wa Lissu, kifungu cha 308 kinazungumzia shahidi mpya, si ushahidi mpya. Alisema upande wa Mashtaka haujaleta shahidi mpya bali unajaribu kuongeza ushahidi kwa shahidi ambaye ushahidi wake tayari ulikamilika kisheria.
“Mlango wa Amini Maamba ulifungwa wakati wa Committal. Kama wanataka ushahidi mwingine, walete shahidi mwingine si kufufua mlango uliokwisha kufungwa,” alisisitiza.
Katika hoja yenye msisitizo mkubwa, Lissu alionya kuwa endapo Notice hiyo itaruhusiwa, Mahakama itakuwa imefungua “sanduku la Pandora.”
Alisema ushahidi unaolengwa unahusisha matukio ya Oktoba 29 matukio ambayo, kwa mujibu wake, hayapo kwenye hati ya mashtaka.
“Ikiwa mtaruhusu hili, mtakuwa mmefungua mlango wa majadiliano mapya nje ya mashtaka yaliyopo. Tutazungumzia mauaji ya Watanzania, tutazungumzia nani aliwajibika kwa vifo vya maelfu. Hili ni balaa la kisheria,”
alionya.
Lissu alisisitiza kuwa yupo tayari kuzungumzia ya Oktoba 29, 2025 huku akiwauliza Mawakili wa Serikali juu ya utayari wao katika kuzungumzia hayo.
Lissu alikwenda mbali zaidi akisema msingi wa hoja za mawakili wa Serikali wanataka kubadilisha hati ya mashtaka ambayo inahusisha matukio ya Oktoba 29, 2025.
“Aprili 3, 2025 ndio tukio lilitokea na Aprili 10, 2025 nikashtakiwa mahakamani, lakini haya maelezo ya ngongeza yanahusu kabla na baada ya uchaguzi” alisema Lissu.
Akongeza ” Ya Oktoba ni magumu, hayahusiki kwa sababu ni maafa na hayatakiwi kuingia hapa ..najaribu majaji kuwasaidia kwa sababu yatatupeleka kusiko, hivyo naomba majaji msikubaliana na notisi hii, yangu ni hayo tu waheshimiwa majaji” Alidai Lissu
Alisisitiza kuwa Notice hiyo ni batili na ni rai yake kwa Mahakama kuifutilia mbali.
Kwa kujibu, Wakili Katuga alieleza kuwa kifungu cha 308 ni msisitizo katika kifungu cha zamani cha 242 (sasa 263), kikilenga kuhakikisha ushahidi wote unaowezekana unawekwa wazi wakati wa Committal.
Alisema kuzuia ushahidi huo sasa ni sawa na kuuzuia usisikike kabisa, jambo ambalo halitendi haki.
Hata hivyo, Lissu alibaki katika msimamo wake akisema:
“Kifungu cha 308 kinahusu shahidi mpya. Hii Notice haihusu shahidi mpya. Kwa hiyo, kisheria ni sawa na sifuri.”
Jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru, linatarajiwa kutoa uamuzi wake kuhusu uhalali wa Notice hiyo, kesho Februari 24 saa tatu asubuhi kisha kuendelea na usikilizwaji wa mashahidi wengine wa Jamhuri.