Kampuni Ya Nishati Ya Orca Kuondoka Tanzania Kufuatia Gharama Kubwa Za Uwekezaji

Kampuni ya Nishati ya Orca (Orca Energy Group Inc.) imetangaza makubaliano ya mwisho ya kuuza shughuli zake nchini Tanzania, hatua inayomaanisha kujiondoa sokoni baada ya zaidi ya miongo miwili. Kampuni hiyo imeeleza kuwa kuendelea na biashara kungehitaji akiba kubwa ya fedha ili kukabiliana na majukumu ya kifedha na matumizi ya mtaji.

Kampuni Ya Nishati Ya Orca Kuondoka Tanzania Kufuatia Gharama Kubwa Za Uwekezaji

Katika taarifa ya Aprili 13, 2026, Orca ilisema: “Kuendeleza miradi ya gesi kungehitaji mtaji mkubwa na dhamana za kifedha ambazo hazipo kwa sasa. Ili kulinda maslahi ya wanahisa wetu, tumelazimika kuchukua hatua ya kimkakati ya kujiondoa.”

Orca ilithibitisha kuwa imeingia mkataba wa mauzo ya hisa na Taifa Gas Tanzania Limited pamoja na Amber Energy Investment L.L.C FZ. Kupitia makubaliano hayo, hisa zote za PAE PanAfrican Energy Corporation (PAEM), kampuni tanzu ya Orca iliyosajiliwa Mauritius, zitauzwa kwa wanunuzi hao. Taifa Gas itanunua asilimia 49 ya PAEM, huku Amber ikipata asilimia 51.

Bodi ya Orca ilieleza kuwa uamuzi huo vile vile uliafikiwa baada ya kutathmini hatari na mashaka yanayohusiana na leseni ya maendeleo ya Songo Songo na mkataba wa kugawana uzalishaji.

“Masharti ya kisheria na kiufundi yamekuwa na changamoto kubwa. Hatari za kisheria na sera za udhibiti zimeongeza shinikizo la kifedha, na kwa hivyo tuliona ni busara kuhamisha mali kwa wawekezaji wapya,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Uuzaji huu unahamisha mali kwa kundi jipya la wanunuzi likiongozwa na Taifa Gas Tanzania Limited, kampuni kinara katika sekta ya gesi nchini. Hatua hii inahakikisha mwendelezo wa shughuli na maendeleo ya mradi huo, huku ikionekana kama fursa ya kuimarisha usalama wa nishati na kuongeza upatikanaji wa gesi kwa soko la ndani.

Orca imesisitiza kuwa kujiondoa kwake kunalenga kulinda fedha kwa ajili ya mgao wa wanahisa na kutimiza mkakati wa muda mrefu wa kupata thamani kutoka kwa mali zake za Tanzania.

“Tunajivunia mchango wetu katika sekta ya gesi ya Tanzania kwa zaidi ya miaka ishirini. Hata hivyo, sasa ni wakati wa kuruhusu wawekezaji wapya kuendeleza mradi huu kwa mtazamo mpya,” ilihitimisha taarifa ya kampuni.

Orca Energy Group Inc. ilijiunga rasmi na sekta ya nishati ya Tanzania mwaka 2004, baada ya kuchukua jukumu la kuendeleza na kuendesha mradi wa gesi wa Songo Songo, ulioko pwani ya kisiwa cha Songo Songo, mkoa wa Lindi. Mradi huo ulikuwa wa kwanza wa kibiashara wa gesi asilia nchini na ulilenga kupunguza utegemezi wa mafuta kwa kuzalisha umeme na kusambaza gesi kwa viwanda na kaya.

Kwa kipindi cha zaidi ya miaka ishirini, Orca imekuwa ikihusiana na uzalishaji wa gesi asilia, ikisaidia kuimarisha sekta ya umeme na kuchochea ukuaji wa viwanda.