Milipuko miwili imeripotiwa katika mji mkuu wa Kampala Jumanne 16 na kuwaua watu watatu na kuwajeruhi wengine 33 katika kisa ambacho polisi wanataja kuwa mashambulizi dhidi ya mji huo. Milipuko ya leo imekuja baada ya msururu wa milipuko mingine kutokea nchini humo mwezi jana.
“Tunachoweza kusema ni kuwa hili lilikuwa shambulio lakini aliyehusika na shambulizi hilo bado hatujamjua,” alisema Msaidizi wa Inspekta Jenerali wa polisi wa Uganda Edward Ochom.
Msemaji wa wizara ya Afya Ainebyoona Emmanuel amesema kwenye Twitter kuwa hospitali ya Mulago imepokea waathiriwa 24 wa mashambulizi hayo, wanne wakiwa katika hali mahututi.
“Kufuatia kitendo hicho cha kigaidi, wahudumu wetu wa afya wanafanya kazi usiku kucha kuokoa maisha ya waliojeruhiwa.”
“Mlipuko wa kwanza ulitokea karibu na kituo cha polisi na mwingine karibu na majengo ya bunge ambapo magari yaliyokuwa karibu yaliteketea moto,” Ochom amesema.
Milipuko miwili iliyotokea leo inafuatia milipuko mingine iliyoripotiwa mwezi jana, wakati bomu lilipolipuka kwenye basi na kuwajeruhi watu kadhaa na mlipuko mwingine uliotokea katika mgahawa na kumuua mwanamke mmoja.
Polisi walisema kuwa mashambulizi hayo mawili ya mwezi jana yalitekelezwa na kundi la Allied Democratic Forces (ADF) kundi ambalo Amerika ililihusisha na kundi la Islamic State
“Barabara ya kwenda bungeni imefungwa huku watu wakijaribu kuondoka maeneo hayo,” amesema Kyle Spencer Mkurugenzi Mkuu wa Internet Exchange Point
Naibu wa Spika Anita Among amesitisha shughuli za bunge na kuwataka wabunge kusalia nyumbani baada ya shambulizi hilo kutokea karibu na majengo ya bunge.
Majengo hayo yamewekwa chini ya ulinzi mkali, huku askari wakilinda eneo hilo, Ubalozi wa Amerika nchini Uganda umewataka raia wake kuepuka eneo hilo.
“Takriban watu sita wameuawa katika eneo la mkasa na wengine 33 kujeruhiwa”, amesema msemaji wa polisi Fred Enanga, inadaiwa kuwa walipuaji watatu wakujitoa muhanga wamehusika katika mashambuzlizi ya leo.
Kulingana na Enanga, mlipuko wa kwanza ulitokea mwendo wa saa 4:15 karibu na kituo cha polisi na mlipuko wa pili kutokea mwendo wa saa 4:06 katika jengo la Raja Chambers katika barabara ya Parliamentary Avenue.