Idadi ya waliouawa katika maandamano ya hivi punde ya kupinga mapinduzi nchini Sudan mwishoni mwa juma imeongezeka na kufikia wanane, madaktari walisema Jumatatu na kufanya idadi ya waliouawa tangu mwezi uliopita baada ya jeshi kuchukua mamlaka kufikia watu 23.
Vijana watatu walikuwa miongoni mwa wale waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya Jumamosi, maandamano hayo yanayojulikana kama Millions March, yalikabiliwa na ukandamizaji mbaya zaidi tangu mapinduzi ya Oktoba 25.
“Idadi iliyothibitishwa ya waliopoteza maisha yao kupigania demokrasia tangu mapinduzi hadi sasa imefikia watu 23,” ilisema Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan, muungano huru wa matabibu.
Muungano huo wa matabibu uliwataja waandamanaji wote wanane waliouawa, akiwemo msichana wa umri wa miaka 13 ambaye ilisema “alijeruhiwa baada ya kupigwa risasi kichwani nje ya nyumba yao,”
“Zaidi ya watu 200 waliojeruhiwa katika makabiliano na polisi wamepata matibabu, wakiwemo 100 waliojeruhiwa kwa risasi za moto, huku wengine wengi wakijeruhiwa kwa risasi za mpira na moshi wa vitoa machozi.” Muungano ulisema.
Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alitangaza hali ya hatari mnamo Oktoba 25 baada ya kuipindua serikali na kuwazuia viongozi wa kiraia.
Mapinduzi hayo ya kijeshi yalilaaniwa na mataifa mengi kote duniani,huku Sudan ikinyimwa misaada na mataifa yenye nguvu duniani yakitaka kurejeshwa kwa utawala wa kiraia kwa haraka.
Waandamanaji wamejitokeza tangu mapinduzi yalipotekelezwa licha ya kukatika kwa intaneti na huduma za mawasiliano, jambo ambalo lililazimu wanaharakati kusambaza wito wa maandamano kupitia grafiti na jumbe za SMS.
Kituo cha Televisheni cha taifa kimeripoti kuwa polisi 39 wamejeruhiwa vibaya katika makabiliano na waandamanaji siku ya Jumamosi.
Polisi wamewashutumu waandamanaji kwa kushambulia vituo vya polisi, wakisema maandamano hayo “yalianza kwa amani lakini yalikengeuka haraka”
Polisi nao walikana kutumia risasi moto na kuwa hawakutumia nguvu kupita kiasi.
Maandamano ya Jumamosi yalikuja siku mbili baada ya Burhan kutangaza baraza jipya la uongozi wa kiraia na kijeshi kuchukua nafasi ya lile aliloliondoa madarakani.
Baraza jipya linajumuisha wanajeshi na watu kutoka kwa vikundi vya waasi wa zamani kutoka kwa baraza lililoondolewa madarakani.
Umoja wa Mataifa umekosoa hatua ya hivi punde ya kijeshi ya kuunda baraza jipya huku nchi za Magharibi zikisema hatua hiyo, “inatatiza juhudi za kurejesha uongozi wa kidemokrasia nchini Sudan.”
Jenerali Burhan anasisitiza kuwa hatua ya jeshi mnamo Oktoba 25, “haikuwa mapinduzi” bali ni njia ya “kurekebisha serikali ya mpito”.