Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, kimekataa kutambua ripoti ya tume ya uchunguzi iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kikisema mchakato mzima haukuwa huru wala wa haki.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa saa chache baada ya ripoti ya matukio ya oktoba 29 kuwasilishwa kwa Rais, chama hicho kimesema kinaendelea kushikilia msimamo wake wa awali wa Novemba 2025 wa kupinga muundo wa tume hiyo, pamoja na matokeo yake yaliyowasilishwa Aprili 23, 2026 chini ya Jaji mstaafu Mohamed Chande.
”Ndugu samia hana mamlaka ya kimaadili wala kisiasa kuunda chombo cha kuchunguza uhalifu mkubwa uliofanywa na utawala wake dhidi ya raia” ilisoma taarifa hiyo.
CHADEMA inadai kuwa ripoti hiyo haiwezi kuchukuliwa kama nyaraka huru, ikisema hata rais mwenyewe amewahi kueleza kuwa ni ripoti yake binafsi. Kwa mtazamo huo, chama hicho kinasema haiwezi kuwakilisha ukweli wala kutoa haki kwa wahusika wa matukio yaliyochunguzwa.
Kimeongeza kuwa uchaguzi uliomweka madarakani Rais Samia Suluhu Hassan haukukidhi viwango vya kidemokrasia, kikirejea tathmini za waangalizi wa kimataifa akiwemo Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Chama hicho pia kimenukuu Sheria ya Tume za Uchunguzi ya mwaka 2002, kikisema kwa mujibu wa sheria hiyo, tume hizo hufanya kazi chini ya mamlaka ya rais na kwa maelekezo yake.
Aidha, chama kimesema haiwezekani kwa mtuhumiwa kujichunguza mwenyewe na kisha kutoa uamuzi wa haki.
Katika kauli yake, CHADEMA imeeleza kuwa serikali ya sasa inahusishwa na matukio mbalimbali ikiwemo mauaji, utekaji, mateso, ubakaji, unyanyasaji na ukiukwaji mpana wa haki za binadamu.
Hata hivyo, serikali haijatoa majibu ya moja kwa moja kuhusu madai hayo yaliyotolewa na chama hicho cha upinzani.
Taarifa hii ya CHADEMA inaongeza mvutano wa kisiasa nchini Tanzania, huku mijadala kuhusu uwajibikaji wa taasisi za umma na uhuru wa vyombo vya uchunguzi ikiendelea kushika kasi.