Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewataja magaidi watatu waliohusika katika milipuko miwili mjini Kampala siku ya Jumanne tarehe 16 Novemba.
Polisi wamethibitisha kuwa washambuliaji walijilipua kwa kutumia vilipuzi vilivyotengezwa nyumbani mwendo wa saa 4 asubuhi, mmoja katika Kituo Kikuu cha Polisi (CPS) na mwingine kwenye barabara ya Parliamentary Avenue.
Mlipuaji wa kujitoa mhanga aliyejilipua katika makao makuu ya polisi ametambuliwa kama Mansoor Uthman huku aliyejilipua kando na barabara ya Parliamentary ametambuliwa kama Wanjusi abdallah.
Rais Museveni Museveni amefichua kuwa polisi waliweza kumkamata gaidi mwingine aliyetambulika kama Musa Mudasiri katika eneo la Katooke, ambaye alifariki baadaye kufuatia makabiliano na Polisi.
Rais Museveni alisema washambuliaji wa Jumanne walikuwa wa kundi lile lile la magaidi waliomshambulia Waziri wa Uchukuzi wa Uganda Jenerali Katumba Wamalwa, “Hawa wote ni sehemu ya kundi la Allied Democratic Forces (ADF) lililomshambulia Jenerali Katumba mwezi Juni.”
Katika mashambulizi dhidi ya Jenerali Katumba, mashuhuda walieleza kuwa wanaume waliokuwa kwenye bodaboda walilimiminia risasi gari la Waziri huyo na kumuua bintiye na dereva papo hapo.
“Kama nilivyoiambia nchi hapo awali, kwa kumshambulia Jenerali Katumba, magaidi hao walijidhihirisha wakati ambapo miundombinu yetu ya ulinzi imeimarika, ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2018 nilipotoa hotuba Bungeni,”Museveni alisema kwenye taarifa yake kwa twitter
“Tangu mashambulizi dhidi ya Jenerali Katumba watu saba wanaoshukiwa kuwa magaidi wameuawa, 81 wamekamatwa na 3 wameuawa.”
“Magaidi wawili wa leo, kwa hivyo, walikuwa wakikimbia kukamatwa.Tumekuwa tukiwasaka tangu mashambuliaji dhidi ya Katumba.”
Mashambulizi mawili ya bomu nchini Uganda Novemba 16 yalisababisha vifo vya raia 3 na kuwajeruhi watu 33.