Katika kabati la nguo la Nana Owiti, mtangazaji maarufu wa Kenya, makumi ya jezi za Arsenal zinaeleza hadithi ya mapenzi yake yasiyoyumba kwa klabu hiyo.

Uhusiano huo ulianza miaka 20 iliyopita, wakati kikosi cha Arsenal kilipojumuisha wachezaji wengi weusi na kupata umaarufu mkubwa barani Afrika.
“Thierry Henry alinifanya nipende Arsenal kwa sababu kwanza alikuwa mtanashati,” alisema Owiti, akiongeza kuwa jezi yake ya kwanza na ya thamani zaidi ni namba 14 ya Henry. “Halafu nikawaona Sol Campbell na Kolo Touré… wachezaji wengi wenye asili ya Kiafrika.”
Mnamo Septemba 2002, Arsenal iliweka historia kwa kuanza na wachezaji tisa weusi katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Leeds, wakishinda 4–1. “Walionekana kama mimi… ndiyo maana nilichagua Arsenal,” alisisitiza Owiti.
Shabiki mwingine kutoka Zimbabwe, Leslie, alikumbuka: “Nilikuwa na miaka 12. Arsenal mara nyingine walikuwa na wachezaji tisa weusi kati ya 11. Niliweza kujitambulisha nao.”
Umaarufu wa Arsenal barani Afrika hauwezi kutenganishwa na mchango wa kocha Arsène Wenger, ambaye mashabiki wanamkumbuka kama kiini cha mvuto wa klabu hiyo.
Emeka Cyriacus Onyenuforo, mwanzilishi na rais wa chama cha mashabiki wa Arsenal nchini Nigeria, alisema umaarufu huo uliongezeka zaidi baada ya nyota wa ndani Nwankwo Kanu kujiunga na Gunners. “Wenger aliifanya Arsenal kuwa klabu iliyounganishwa, bila kuangalia rangi ya mchezaji, bali akatafuta vipaji kutoka popote na kuwainua hadi kuwa wachezaji maarufu,” alisema Onyenuforo.
Nchini Ethiopia, Akalework Amde, mwenyekiti wa chama cha mashabiki, alisisitiza kuwa Wenger alionekana “kuwapa kipaumbele wachezaji wa Kiafrika.”
Katika kipindi hicho, Arsenal walipata mafanikio makubwa: mataji matatu ya Ligi Kuu (1998, 2002, 2004) na rekodi ya kutopoteza mechi 49 mfululizo mnamo 2003–2004, iliyowapa jina la “The Invincibles.”
Huo ulikuwa wakati ambapo Ligi Kuu ya England iligeuka kuwa chapa ya kimataifa, ikipeperushwa katika nyumba za Waafrika kupitia kituo cha Supersport. “Ukirudi miaka ya 80, kila Mkenya alitazama soka la Ujerumani, kwa sababu ndilo pekee lililokuwa likionekana,” alisema Carol Radull, mtangazaji na shabiki maarufu wa Arsenal.
Hata baada ya miongo ya ukame wa mataji, mapenzi hayajapungua. Hayati Raila Odinga, kiongozi wa kisiasa wa Kenya, alikuwa shabiki wa dhati, huku Rais wa Rwanda Paul Kagame akiendeleza uhusiano kupitia kampeni ya “Visit Rwanda.”
Kwa sasa, mashabiki wanapenda Arsenal si kwa sababu ya rangi ya wachezaji pekee, bali kwa klabu yenyewe. “Sasa watu wanapenda timu kwa sababu ya timu,” alisema Robbie Lyle, mwanzilishi wa Arsenal Fan TV. “Mashabiki wamekuwa wa ajabu kabisa. Afrika, kila mahali unapoenda, unaona jezi ya Arsenal.”
Leo, Arsenal imekuwa zaidi ya klabu ya soka — ni utambulisho wa kifahari wa Kiafrika, na kila kona ya bara huonekana jezi nyekundu za Gunners zikipeperushwa kwa fahari.