Habari njema kwa mashabiki wa nyota wa muziki kutoka Nigeria P Square, baada ya habari kuchipuka kuwa baada ya miaka mitano wasanii hao watarejea na kutoa nyimbo pamoja. Uvumi kuhusu kuungana kwao ulianza kuenea mapema wiki hii.
Jumatano Novemba 18, 2021 wawili hao walionekana kwa mara ya kwanza wakiwa pamoja katika video iliyosambaa kwenye mtandao ya kijamii wa Instagram.
Katika mkesha wa siku yao ya kuzaliwa ya 40, video ya wawili hao wakikumbatiana ilisambaa, ikithibitisha kuwa ndugu hao wamerudiana. Katika video hiyo Paul anaonekana akiingia ndani ya nyumba ya kifahari na kumfuata Peter kisha kumkumbatia huku akiwa anamshagaa.
Mashabiki walipokea taarifa za kuungana kwao kwa shangwe huku wengi wakisubiri kwa muda mrefu kuona mapacha hao wakipatana na kurudisha ladha ya muziki iliyowafanya kuwa nyota wa muziki barani Afrika.
P Square ikiwa ni pacha Peter na Paul walianza kupata umaarufu baada ya kutoa albamu yao ya kwanza “Last Nite” mnamo mwaka wa 2001. Kufikia 2005 walipotoa albamu yao ya pili “Get Squared” walikuwa wamekuwa nyota Afrika. Wawili hao waliendelea kupaa na kujizolea umaarufu wakifunga dili na kushinda tuzo hadi 2016 walipoachana kufuatia kutoelewana kuhusu usimamizi wao.
Inasemekana kuwa chanzo cha kusambaratika ni malalamiko kutoka kwa Peter kutaka mabadiliko katika uongozi kwa madai kuwa kundi lilionekana la kifamilia zaidi kuliko kibiashara.
Jambo hilo, Paul hakuliafiki na hapo ndipo kikawa chanzo cha kundi hilo kuvunjika na kila mtu aliamua kufanya kazi kivyake ambapo Paul alianza kutumia jina la Rudeboy na kuanzisha lebo yake ya ‘Rudeboy’ huku Peter akijiita Mr P na kutangaza uongozi wake mpya.
Wakiwa pamoja walitawala tasnia ya muziki wa Nigeria kwa miaka mingi, tamasha na maonyesho yao yakihudhuriwa na wengi. Walishirikiana na wasanii kama vile Diamond Platinumz wa Tanzania na supastaa wa Marekani Akon. Walisajiliwa kwenye lebo ya Akon ya Konvict Muzik mwaka wa 2011 na kisha mwaka mmoja baadaye wakapata mkataba wa usambazaji na Universal Music Group. Pamoja na kutajwa kuwa Msanii Bora wa Muongo wa MTV Africa mwaka 2015 walishinda taji la Kundi Bora mara tatu.
Juhudi za wengi kuwapatanisha wawili hao hazikuzaa matunda hadi hivi majuzi.
Ili kuadhimisha siku yao ya kuzaliwa, ndugu hao walituma salamu za siku ya kuzaliwa kwa kila mmoja kwenye mtandao wa Instagram. Paul, hata hivyo, alichukua hatua zaidi kwa kuchapisha picha ya kikundi hicho pamoja na nambari ya akaunti na nukuu:
“Starting from @obi_cubana and @judeengees even @davido 😂 let’s show @davido that 2 heads are better than 1☝🏽… .. everything na double double❤️🍾🎉”