Kesi ya Lissu: Shahidi Akiri Kutoeleza Tofauti ya Ushahidi wa Maelezo ya Polisi na Aliotoa Mahakamani

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, imeendelea leo mahakamani, huku Lissu akimaliza kumuuliza maswali ya dodoso shahidi wa upande wa Jamhuri, ACP Amini Mahamba, kuhusu tofauti zilizopo kati ya maelezo aliyoyatoa kwa polisi na ushahidi alioutoa mahakamani.

Kesi ya Lissu: Shahidi Akiri Kutoeleza Tofauti ya Ushahidi wa Maelezo ya Polisi na Aliotoa Mahakamani

Katika mahojiano hayo, Lissu pia alimuuliza shahidi kuhusu watu waliokamatwa kwa tuhuma za kupanga kuvuruga uchaguzi lakini baadaye kutofunguliwa mashtaka, madai kuhusu vifo vilivyotokea katika baadhi ya mikoa baada ya uchaguzi, pamoja na ushahidi wa video unaohusishwa na kesi hiyo.

Haya ni baadhi ya yaliyojiri mahakamani

Lissu: Shahidi, nataka kwanza nianze na maswali yangu ya jana kuhusu tofauti kati ya ushahidi ulioutoa kwenye maelezo ya polisi na ushahidi ulioutoa kizimbani. Waeleze Waheshimiwa Majaji kama unaamini maelezo yako yanapaswa kuaminiwa na mahakama.Shahidi: Ni kweli.Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji kama kuna mahali umeeleza sababu za tofauti kati ya ulichoandika na ulichosema mahakamani.Shahidi: Hakuna mahali.Lissu: Unakumbuka ulisema mashahidi hao ni watu waliokamatwa na polisi kwa kupanga kuhamasisha kuvuruga uchaguzi?Shahidi: Kweli.Lissu: Walipokamatwa walikiri kwa polisi kwamba walikuwa wanapanga mipango hiyo na wakaandika maelezo?Shahidi: Kweli.Lissu: Hiyo mipango waliyopanga ilikuwa mipango ya jinai, kweli si kweli?Shahidi: Kweli.Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, tuhuma hizo za kijinai mlizowakamata nazo ziliishia wapi?Shahidi: Baada ya kupitia mahojiano yao, ilibainika kwamba walikuwa wanaelekezwa na wewe.Lissu: Kwa hiyo ni kweli mliwafutia wote kesi?Shahidi: Kweli.Lissu: Katika hao watu waliokuja kutoa ushahidi wa kificho, wapo waliotokea Arusha?Shahidi: Kweli.Lissu: Mliwafutia kesi?Shahidi: Hawakuwa sehemu ya mashtaka.Lissu: Kuna watu mliowakamata Mbeya, wakakiri kupanga maafa kwenye uchaguzi na wakaandika maelezo, mkawaleta mahakamani, halafu mkawafutia mashtaka yao?Shahidi: Kweli.-Kuhusu vifo na hatua dhidi ya viongozi-Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji kama katika hiyo mikoa mitatu, ambako jumla ya watu waliouawa ni 315 kwa mujibu wa ripoti ya Jaji Chande, RPC na Wakuu wa Mikoa walichukuliwa hatua.Shahidi: Sina uhakika.Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji, wale waliopanga kufanya vurugu, kuna yeyote ambaye mmemkamata mpaka sasa?Shahidi: Hayupo.Lissu: Sasa kuna mikoa mingine minane. Mkoa wa Mwanza hawakukuletea taarifa kama kuna fujo?Shahidi: Hawakupata taarifa.Lissu: Niambie kama niko sahihi ama nakosea kwamba katika historia yetu, mara ya mwisho watu waliuawa kwa wingi ilikuwa mwaka 1907. Tangu hapo hapakuwa na idadi kubwa ya watu kuuawa kama ilivyokuwa mwaka jana. Ndani ya wiki moja ya utawala wa Samia, watu zaidi ya 500 wameuawa.Shahidi: Hauko sahihi.-Kuhusu video ya ushahidi-Lissu: Kwenye ushahidi wako kuhusiana na video, ulisema wewe na timu yako mlikaa mkaangalia video yote. Video mliyoangalia ilikuwa ile iliyokuwa mitandaoni au ile ya kwenye flash?Shahidi: Ile iliyokuwa kwenye mtandao.Lissu: Kwa hiyo, hamkuangalia video inayodaiwa kuwa kwenye flash inayoitwa Aldivo?Shahidi: Hatukuangalia.Lissu: Nitakuwa sahihi nikisema kwamba kwenye hiyo flash pengine hakukuwa na video?Shahidi: Ipo.Lissu: Unajuaje?Shahidi: Nimefahamu kupitia taarifa ya mchunguzi.Lissu: Hiyo taarifa ipo mahakamani?Shahidi: Ipo.Lissu: Ilikataliwa. Kwenye hilo swali, wewe ni shahidi wa 16, na nyie wote kuanzia shahidi wa kwanza mpaka wewe, hakuna yeyote aliyewasilisha ushahidi wa taarifa wala video upande wa mashtaka. Hamjaleta chochote.Shahidi: Sina uhakika.-Kuhusu Katiba mpya na madai ya mfumo huru wa uchaguzi-Lissu aliendelea kumuuliza shahidi kama anafahamu historia ya madai ya Katiba mpya na mfumo huru wa uchaguzi nchini, akieleza kuwa hoja hizo zimekuwa zikijadiliwa kwa miaka kadhaa.Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji kama unafahamu kwamba madai ya Katiba mpya na mfumo huru wa uchaguzi ni madai ambayo yamekuwepo kwa muda wa miaka 35.Shahidi: Sifahamu.Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji kwamba mwaka 1990 Tume ya Nyalali ilipendekeza Katiba mpya itungwe mwaka 2003.Shahidi: Sifahamu.Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji kwamba mwaka 1998 Rais Benjamin Mkapa aliunda Tume iliyoongozwa na Jaji Robert Kisanga, ambayo ilipendekeza kuwe na Katiba mpya.Shahidi: Sifahamu.Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji kama unafahamu kwamba watazamaji wa uchaguzi kutoka nje wamekuwa wakipendekeza kwa Serikali itungwe Katiba mpya ili kuondoa matatizo ya uchaguzi.Shahidi: Sifahamu.Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji kama unafahamu kwamba mwaka 2015, kwenye uchaguzi mkuu, ilani ya CCM ilikuwa na ahadi ya kumaliza mchakato wa Katiba mpya.Shahidi: Sifahamu.Lissu: Na kama unafahamu kwamba baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani alisema hakuna Katiba mpya.Shahidi: Sifahamu.-Lissu auliza kuhusu kauli za taasisi za kimataifa-Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji kama unafahamu kwamba tarehe 13 Februari mwaka huu, kikosi kazi cha Kamati ya Haki za Binadamu kinachoshughulikia masuala ya watu wanaokamatwa na kubambikiwa kesi kilitoa taarifa kwamba kukamatwa kwangu ni kukiuka sheria na kupendekeza niachiliwe huru pamoja na kulipwa fidia.Shahidi: Sifahamu.Lissu: Waeleze Waheshimiwa Majaji kama unafahamu kwamba mwezi uliopita, tarehe 10 Julai, Kamati ya Mawaziri wanaowakilisha Jumuiya ya Madola ilitaka Tanzania iniachilie huru bila masharti ndani ya siku 30, na ikasema Serikali isipofanya hivyo, kikao cha Septemba kitashughulikia suala hilo.Shahidi: Sifahamu.Baada ya maswali ya Lissu, upande wa Serikali kupitia Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, uliomba ufafanuzi kuhusu baadhi ya majibu ya shahidi, hasa tafsiri ya kauli inayodaiwa kutolewa na Lissu kuhusu “kuzuia uchaguzi”, maana ya neno Serikali katika kauli hiyo na uhusiano kati ya madai ya Katiba mpya na shtaka linalomkabili.Wakili Katuga: Uliulizwa hapa kuhusiana na yale maneno yanayosemekana kusomwa na mshtakiwa kwamba, “tutazuia uchaguzi.” Ulipoulizwa kwamba neno “Serikali” lipo, ukasema lipo. Ulimaanisha nini?Shahidi: Nilimaanisha kwamba Serikali ndiyo yenye wajibu wa kutekeleza na kusimamia sheria za nchi. Kwa hiyo, kutamka maneno kama hayo kwamba “tutazuia uchaguzi” maana yake ni kuitishia Serikali na kuvuruga amani ya nchi.Wakili Katuga: Uliulizwa nani aliyechapisha maneno haya mtandaoni, ukasema ni wewe mshtakiwa. Ulimaanisha nini?Shahidi: Nilimaanisha kwamba mshtakiwa ndiye aliyekuwa akiongea mbele ya wale waandishi wa habari, ambapo waandishi walikuwa wakirusha taarifa hizo.Wakili Katuga: Umeulizwa tena kifungu cha 39(2)(b) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16. Ulipoulizwa kama maneno ya “kuzuia uchaguzi” yamo kwenye kifungu hicho, ulisisitiza yamo. Ulikuwa unamaanisha nini?Shahidi: Kifungu cha 39 kimeandikwa kwa nia ya kuitishia Serikali. Kwa hiyo, yale maneno ambayo amesema mtuhumiwa, tafsiri yake ni kwamba alimaanisha kuitishia Serikali.Wakili Katuga: Umeulizwa sana hapa kuhusiana na Katiba na ukaulizwa kudai Katiba kunahusiana vipi na kesi hii. Ifafanulie mahakama haya madai ya Katiba na kosa la uhaini katika hili.Shahidi: Hayahusiani.Wakili Katuga: Uliulizwa kwamba wewe na timu yako mlifanya vurugu, ukasema si kweli. Fafanua.Shahidi: Si kweli kwa sababu uchunguzi ulibaini wazi kwamba vurugu zile zilifanywa kutokana na uchochezi, kwa sababu palikuwepo maandalizi ya vurugu hizo kabla ya Oktoba 2025.Wakili Katuga: Umeulizwa kuhusu ushahidi ulioutoa mahakamani na kielelezo cha maelezo yako. Umeulizwa kama unataka ushahidi wako uaminiwe mahakamani. Lakini ukaulizwa kwamba uliandika sababu za maelezo yako kutofautiana na ya polisi na ya hapa mahakamani, ukasema hapana.Shahidi: Waheshimiwa, ni kweli sijaeleza. Ninachofahamu ni kwamba maelezo niliyotoa ofisini na niliyotoa hapa yametokana na jinsi nilivyoulizwa swali hapa.

-Kesi yaahirishwa-Baada ya shahidi Mahamba kumaliza kutoa ushahidi wake, Mahakama ikaahirisha kesi hiyo hadi kesho Agosti 13, 2026 saa  tatu asubuhi, wakati ambapo mwenendo wa shauri utaendelea kwa hatua ya usikilizwaji wa shahidi wa 17 wa Jamhuri.