Shahidi Akwamisha Kesi ya Lissu, Mahakama Yaahirisha hadi Jumatatu

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, imeahirishwa hadi Jumatatu, Agosti 17, 2026, baada ya upande wa Jamhuri kueleza kuwa shahidi aliyepangwa kutoa ushahidi leo amepata dharura ya kiafya.

Shahidi Akwamisha Kesi ya Lissu, Mahakama Yaahirisha hadi Jumatatu

Kesi hiyo imefikia hatua hiyo leo Ijumaa, Agosti 14, 2026, baada ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ajuaye Nzegeli, kuiomba Mahakama kuahirisha usikilizwaji kwa sababu shahidi aliyekuwa amepangwa kufika mahakamani amekwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kliniki.
“Waheshimiwa Majaji, shauri limekuja kwa ajili ya kusikilizwa. Shahidi wetu tuliyeandaa leo amepata dharura ya kiafya, amekwenda Muhimbili kuhudhuria kliniki yake. Kwa hiyo tunaomba shauri liahirishwe mpaka Jumatatu ambapo tutaleta mashahidi wetu,” alisema Nzegeli.

Hata hivyo, Lissu ambaye anajiwakilisha mwenyewe katika kesi hiyo, alipinga ombi hilo akisema yuko tayari kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo.

Lissu alidai kuwa upande wa Jamhuri umekuwa ukikiuka amri ya Mahakama iliyowataka kuwasilisha angalau mashahidi wawili kila siku kesi inapopangwa kusikilizwa.

“Waheshimiwa Majaji, kwanza niseme kwamba mimi niko tayari kuendelea na kesi leo. Na pili, ninapinga ombi la kuahirisha kesi hii kwa sababu iliyotolewa na mawakili wa Serikali,” alisema Lissu.

“Waheshimiwa Majaji, kulikuwa na amri mliyotoa mwaka jana kwamba upande wa mashtaka ulete mashahidi wasiopungua wawili kila siku ambapo kesi hii inaposikilizwa. Na hii amri mmeirudia tena juzi Jumatano, mmeirudia jana kwamba upande wa mashtaka walete mashahidi wengi.”

Lissu ameendelea kupinga kuahirishwa kwa kesi hiyo akidai kuwa upande wa Jamhuri umekuwa ukiomba kuahirishwa kwa kesi mara kwa mara bila Mahakama kuchukua hatua dhidi yao.

“Sasa, Waheshimiwa Majaji, upande wa mashtaka hawatekelezi amri ya Mahakama kwa sababu wanajua mtashindwa kuwachukulia hatua. Samahani sana. Wanafanya hivi kwa sababu hawatachukuliwa hatua. Yanayotokea haya ni kwa sababu mliyoyatoa yanapuuzwa, hamjachukua hatua kabisa,” alisema.

Lissu pia aliitaka Jamhuri kufikiria kuondoa kesi hiyo endapo imeshindwa kuendelea na ushahidi kwa kasi inayotarajiwa, akisema kucheleweshwa kwa kesi hiyo kunasababisha muda mwingi kupotea huku akiwa bado anashikiliwa gerezani.

“Kwa hiyo kama wanaona hii kesi haiendelei, waitoe,” alisema Lissu.

Akirejea kesi ya Khatibu Ghandi na wenzake, Lissu alidai kuwa Mahakama za Tanzania tayari zimewahi kukabiliana na mazingira ya kesi iliyochukua muda mrefu na kwamba kuna historia ya maamuzi yanayohusu umuhimu wa kesi za jinai kuendeshwa bila ucheleweshaji usio wa lazima.

“Hii njia ilifagiliwa tangu mwaka 1982/83. Khatibu Ghandi na wenzake, kati ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, kesi ilichukua mwaka mmoja na siku 17. Na haya ninayoyasema, Waheshimiwa Majaji, yapo kwenye rekodi za hizo kesi,” alisema.

Lissu pia amehoji muda ambao kesi hiyo imechukua hadi sasa, akisema imefikia takribani siku 493, huku upande wa Jamhuri ukiwa umewasilisha mashahidi 17 kati ya 30 waliopangwa kutoa ushahidi.

Kwa upande wake, Wakili Mkuu wa Serikali Ajuaye Nzegeli alikiri kuwa Jamhuri bado ina mashahidi wengi, lakini akasema uwepo wa mashahidi hao haupaswi kutafsiriwa kwamba wote lazima waitwe kwa wakati mmoja au katika kila siku ya usikilizwaji.

“Tumesikia mwenzetu. Mashahidi, Waheshimiwa Majaji, nao ni binadamu na kwa kuwa ni binadamu changamoto inaweza kutokea muda wowote,” alisema.

“Sisi upande wa mashtaka tunakiri kwamba tuna mashahidi wengi, lakini si lazima tulete mashahidi wote. Ni kwa jinsi tulivyopanga kwamba tulete shahidi gani. Pengine labda huyu ni shahidi wa mwisho.”

Nzegeli alisisitiza kuwa sababu ya kiafya iliyotolewa na shahidi huyo ni ya msingi na kuiomba Mahakama iruhusu kesi hiyo kuahirishwa hadi Jumatatu.

“Kwa sababu za maradhi sisi tumeona ni za msingi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Majaji, ni rai ya Jamhuri kwamba tunaomba Mahakama yenu ituahirishie mpaka Jumatatu ambapo tutaleta mashahidi wetu,” alisema.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, jopo la Majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru limekubali ombi la upande wa Jamhuri na kuahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu, Agosti 17, 2026, saa 3:00 asubuhi.

Katika uamuzi wake, Mahakama imesema imezingatia hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili, ikiwemo sababu ya kiafya iliyotolewa na upande wa mashtaka na pingamizi la Lissu dhidi ya kuahirishwa kwa kesi hiyo.

Lissu alisisitiza umuhimu wa Mahakama kusimamia amri zake, akisema kesi hiyo ni miongoni mwa kesi kubwa zaidi zinazofuatiliwa nchini kutokana na aina ya shtaka linalomkabili.

“Hii ndiyo kesi kubwa kuliko zote kwa mujibu wa Katiba hii. Huo umuhimu wa hii kesi ni lazima Mahakama isimamie amri zake. Bahati nzuri, Waheshimiwa Majaji, hatutembei njia ambayo haijafagiliwa,” alisema Lissu.

Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini, ambalo ni miongoni mwa makosa makubwa zaidi ya jinai chini ya sheria za Tanzania na linaweza kubeba adhabu ya kifo endapo mshtakiwa atapatikana na hatia.