Lissu: Jamhuri Imeshindwa Kuthibitisha Kesi, Naomba Mahakama Itamke Sina Kesi ya Kujibu

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, amesema upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha msingi wa shtaka la uhaini linalomkabili, akiiomba Mahakama Kuu itamke kuwa hana kesi ya kujibu.
Lissu: Jamhuri Imeshindwa Kuthibitisha Kesi, Naomba Mahakama Itamke Sina Kesi ya Kujibu

Lissu ameyasema hayo leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wake uliowasilishwa kupitia mashahidi 17, akisisitiza kuwa ushahidi uliotolewa haujafikia kiwango cha kumtaka aanze kujitetea.Akiwasilisha hoja yake ya “No Case to Answer”, Lissu amesema Jamhuri imeshindwa kuthibitisha kuwepo kwa nia ya kutenda uhaini pamoja na vitendo vinavyothibitisha nia hiyo.

Kwa mujibu wa Lissu, ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka haujaonyesha kwa kiwango kinachotakiwa kisheria kwamba alifanya vitendo vinavyounda kosa la uhaini kama linavyodaiwa katika hati ya mashtaka.
Amesema pia kuwa endapo ushahidi uliotolewa na Jamhuri hauwezi, hata ukiachwa bila kupingwa na upande wa utetezi, kupelekea Mahakama kumtia hatiani, basi hakuna msingi wa kumtaka yeye kuanza kujitetea.Kwa msingi huo, Lissu ameiomba Mahakama kutumia kifungu cha 312(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na kutamka kuwa hana kesi ya kujibu, badala ya kumtaka kuingia katika hatua ya utetezi.Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, chini ya jopo la majaji watatu, sasa inatarajiwa kupitia hoja za pande zote mbili pamoja na ushahidi uliotolewa kabla ya kutoa uamuzi kuhusu iwapo Lissu ana kesi ya kujibu au la.Lissu, mwenye umri wa miaka 58, ni mmoja wa wanasiasa wanaotajwa kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za upinzani nchini Tanzania. Mwanasheria huyo aliingia Bungeni mwaka 2010 kama Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chadema na baadaye akawa mmoja wa wakosoaji wakuu wa serikali. Pia amewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) na tangu Januari 2025 ni Mwenyekiti wa Chadema.Ushawishi wake pia umevuka mipaka ya Tanzania, huku akiwa sehemu ya mijadala ya kimataifa kuhusu demokrasia, utawala bora na mageuzi ya kisiasa.Lissu si mara ya kwanza kukabiliwa na kukamatwa au kuzuiliwa kutokana na shughuli zake za kisiasa. Mwaka 2017 pekee alikamatwa mara kadhaa, kabla ya kushambuliwa kwa risasi Septemba mwaka huo na kulazimika kwenda Kenya na baadaye Ubelgiji kwa matibabu.Hata hivyo, kesi ya sasa ya uhaini ndiyo imepelekea Lissu kukaa gerezani kwa muda mrefu zaidi katika historia yake ya kisiasa. Alikamatwa Aprili 9, 2025, na hadi leo, Agosti 17, 2026, amekuwa kizuizini kwa zaidi ya miezi 16 akisubiri mchakato wa kesi hiyo. Sasa, baada ya Jamhuri kufunga ushahidi wake, macho yanaelekezwa kwa Mahakama kuona kama ushahidi huo umeweka msingi wa Lissu kuwa na kesi ya kujibu, au kama Mahakama itakubaliana na hoja yake kwamba hana kesi ya kujibu uamuzi ambao unatarajiwa kutolewa Agosti 21,2026 siku ya Ijumaa saa tatu asubuhi