Wazo la kuwepo kwa “15 minute city” ambapo wakaazi wote wanaweza kufikia sehemu zao kazi na maeneo ya burudani ndani ya robo saa kwa kutembea au kuendesha baiskeli kutoka majumbani mwao limepata msukumo mkubwa kati ya wapangaji wa miji wakati wa janga la UVIKO-19.
Sasa, kikundi cha wasanifu majengo kinapanga ujenzi wa mji wa “10 minute city” katika mji mkuu wa Korea Kusini, Seoul.
Mradi huo unaofahamika kama “Project H1” unatarajiwa kubadilisha viwanda vya zamani kuwa jiji “janja”.
Jiji hilo litajumisha majengo manane ya makazi na majumba ya ofisi pamoja na shule. Mradi huo wa ekari 125 pia utakuwa na kumbi za burudani, vituo vya mazoezi ya mwili, mabwawa ya kuogelea na hata mashamba ya mijini ya “hydroponic”.
Jiji hilo liliuundwa na kampuni ya usanifu ya Uholanzi ya UNStudio na kuungwa mkono na Kampuni ya Maendeleo ya Hyundai. Hakutakuwa na gari hata moja Jijini humo.
Taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu mradi huo ilidai kuwa “mahitaji yote yanayoyohitajika mijini yatapatikana kwa urahisi na kwa haraka jijini humo ndani ya umbali wa dakika 10 kutoka kwa makazi ya watu.”
Dhana ya “15 minute city” ilipendekezwa kwa mara ya kwanza na msomi wa Kifaransa-Colombia Carlos Moreno mwaka wa 2016, na kupigiwa debe na meya wa Paris Anne Hidalgo, ambaye alipendekeza kuufanya mji mkuu wa Ufaransa kuwa “mji wa robo saa “wakati wa kampeni yake ya kuchaguliwa tena kuwa meya wa Paris Ufaransa.
Janga la UVIKO -19 limeongeza umaarufu wa mradi huu wa “mji wa dakika 15”, huku watu wengi duniani wakiendelea kufanya kazi nyumbani na kuepuka usafiri wa umma, wapangaji wa miji wameanza kufikiria upya jinsi miji itakavyoweza kudhibiti ongezeko la idadi ya watu.
Moreno aliongeza kuwa “utafiti zaidi sasa unastahili kuonyesha jinsi wazo hilo na vipengele vyake vinaweza kuigwa katika miji mingine kote duniani.”