
Kabla ya hatua hiyo, Mahakama imesikiliza hoja na pingamizi zilizowasilishwa na pande zote kuhusu mashahidi wa upande wa utetezi.
Upande wa Jamhuri umeeleza kuwa hauna pingamizi kwa mashahidi wa namba 8 hadi 11 kuendelea kutoa ushahidi.
Jamhuri pia imeeleza kuwa inakubaliana na matumizi ya Kifungu cha 314 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinachoruhusu mashahidi hao kuendelea na utoaji wa ushahidi wakati Mahakama ikiendelea kujiandaa kutoa uamuzi.
Hata hivyo, Lissu ameomba Mahakama impe muda mfupi ili aweze kuzungumza na mashahidi hao kabla ya kuendelea na hatua ya kujitetea.
Lissu ameiambia Mahakama kuwa hajaonana na mashahidi hao tangu Novemba 2025, hivyo anaona ni muhimu kupata nafasi ya kukutana nao na kujadiliana nao kabla ya kuendelea na mwenendo wa kesi.
Lissu amesema, “Niliomba nipate fursa ya kuonana nao. Sijaonana nao hao mashahidi tangu Novemba 2025, hivyo naomba Mahakama inipe ahirisho fupi ili niweze kujadiliana nao kabla ya kuendelea.”
Akizungumzia ombi hilo, Lissu amesema yeye ni mtu ambaye ni “sensitive sana” katika suala la kuahirisha kesi, akieleza kuwa hatamani mwenendo wa kesi kucheleweshwa.
“Sasa kama kuahirisha hivi, mimi nitaenda gerezani, hivyo naomba nipate health break ili nishauriane na wenzangu halafu tuendelee,” amesema Lissu.
Jaji ameieleza Mahakama kuwa kikao kiliahirishwa kwa muda mfupi, kuanzia saa 8:11 mchana hadi saa 9:30 mchana, ili Lissu apate fursa hiyo ya kushauriana na wenzake.
Baada ya mapumziko hayo, Lissu anatarajiwa kuendelea na hatua ya kuanza kujitetea katika kesi hiyo, huku Mahakama ikiwa bado inasubiri kutoa uamuzi kuhusu pingamizi lililowasilishwa na upande wa Jamhuri.
Katika hatua hii Lissu atawahoji mashahidi wake ambao hawajawekewa pingamizi na Serikali ambao ni Katibu Mkuu, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara Amani Golugwa, Makamu Mwenyekiti wa Chadema John Heche, na Mkurugenzi wa Idara ya Mawasilisho Brenda Rupia huku yeye mwenyewe akiwa Shahidi namba moja.