Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ameanza kujitetea mwenyewe katika kesi ya uhaini inayomkabili, baada ya Mahakama Kuu kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa utetezi.

Lissu amekuwa shahidi wa kwanza wa utetezi na ameanza kutoa ushahidi wake chini ya kiapo, akieleza kuwa hajawahi kutoa ushahidi mahakamani na hivyo kuomba aongozwe katika hatua hiyo.
“Natoa ushahidi chini ya kiapo lakini naomba niongozwe kwa sababu sijawahi kutoa ushahidi. Nimeshtakiwa mara nyingi kuliko hesabu lakini sijawahi kufikia hatua hii,” amesema Lissu.
Katika ushahidi wake wa awali, Lissu ameeleza historia yake ndani ya CHADEMA, akisema amekuwa katika uongozi wa juu wa chama hicho kwa takribani miaka 20 na kwa sasa ni Mwenyekiti wa chama hicho, nafasi aliyoanza kuishikilia Januari 21, 2025.
Amesema alikaa katika nafasi hiyo kwa takribani wiki tano kabla ya kushtakiwa kwa kosa la uhaini.
Lissu pia ameeleza historia yake ya kisiasa na ubunge, ikiwemo kuwa Mbunge wa Singida Mashariki, pamoja na nafasi mbalimbali alizowahi kushikilia ndani ya CHADEMA na katika uongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Katika sehemu ya ushahidi wake, Lissu amerejea tukio la kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 akiwa Dodoma, akisema baada ya shambulio hilo alipelekwa Nairobi, Kenya, na baadaye Ubelgiji kwa matibabu.
Amesema alifanyiwa jumla ya operesheni 25, zikiwemo 17 Nairobi na nane Ubelgiji, akieleza kuwa madhara ya shambulio hilo ndiyo sababu ya kutembea kwa kuchechemea.
Lissu pia amezungumzia uzoefu wake katika uchaguzi, akisema ameshiriki katika chaguzi nyingi Tanzania kama mpiga kura au mgombea, isipokuwa uchaguzi wa mwaka 2000 alipokuwa akifanya kazi Marekani na uchaguzi wa mwaka 2025 kwa sababu alikuwa gerezani.
Amesema pia amefanya utafiti kuhusu mfumo wa uchaguzi Tanzania tangu kipindi cha Ukoloni hadi sasa, akidai kwamba kama asingekuwa anashikiliwa katika Gereza la Ukonga, angekuwa tayari amechapisha kitabu kuhusu masuala ya uchaguzi na kile alichokiita “uchafu wake”.
Lissu ameendelea kutoa ushahidi wake kuhusu historia yake, nafasi alizowahi kushikilia na msimamo wake wa kisiasa, huku akisisitiza kuwa kesi inayomkabili inahusiana na kauli aliyoitoa Aprili 3, 2025 kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kwa kuwa muda wa Mahakama umefikia ukomo, Lissu amesitisha ushahidi wake kwa leo na anatarajiwa kuendelea kujitetea Jumatatu, Agosti 24, 2026.