Lissu: “Kesi ya Uhaini ni Mwendelezo wa Kesi za Kisiasa Nilizofunguliwa”

Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, amesema kesi ya uhaini inayomkabili ni mwendelezo wa kesi mbalimbali za kisiasa ambazo amedai amekuwa akifunguliwa na Serikali kwa miaka mingi kutokana na misimamo na shughuli zake za kisiasa.

Lissu: “Kesi ya Uhaini ni Mwendelezo wa Kesi za Kisiasa Nilizofunguliwa”

Lissu ametoa kauli hiyo leo wakati akiendelea kujitetea mwenyewe mbele ya Mahakama Kuu, akieleza historia ya kukamatwa na kufunguliwa kesi katika tawala tofauti za Tanzania.

Amesema katika utawala wa Rais Benjamin Mkapa, alikamatwa Desemba 22, 2002, siku mbili kabla ya Krismasi, kwa tuhuma za uchochezi baada ya kudai uchunguzi kuhusu mauaji ya wananchi wa Bulyanhulu.

Kwa mujibu wa Lissu, kesi hiyo ilidumu kwa miaka sita kabla ya Serikali kuifuta kwa kukosekana kwa ushahidi.

Amesema katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, alikabiliwa tena na kesi baada ya kwenda Nyamongo, Tarime, kufuatia mauaji ya wananchi yaliyodaiwa kufanywa na polisi katika eneo la mgodi.

Lissu amesema alikamatwa katika eneo hilo na baadaye kufunguliwa kesi ambayo nayo, kwa mujibu wake, ilifutwa na Hakimu wa Wilaya baada ya upelelezi kushindwa kukamilika.

Amesema mwaka 2012 alikamatwa tena pamoja na viongozi wengine wa CHADEMA baada ya polisi kuua wananchi katika maandamano, huku kesi hiyo ikiendelea mahakamani bila mashahidi wa upande wa mashtaka kuwasilishwa hadi ilipofutwa.

Ameeleza pia kuhusu kukamatwa kwake mwaka 2013 wakati wa mgogoro wa kisiasa uliotokana na mkutano wa CHADEMA ulioshambuliwa, akisema kesi hiyo ilihusisha tuhuma za mkusanyiko usio halali.

Kwa upande wa utawala wa Rais John Magufuli, Lissu amesema alikamatwa mwaka 2015 baada ya kutoa kauli kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, na baadaye mwaka 2016 na 2017 alikabiliwa na mfululizo mwingine wa kukamatwa na kesi.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2016 hadi Agosti 2017 alikamatwa mara nane na kufunguliwa kesi sita katika Mahakama ya Kisutu.

Lissu pia amerejea tukio la Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa kwa risasi akiwa nje ya makazi yake Dodoma, akisema alinusurika baada ya kupigwa risasi 16 na hadi sasa anaishi na risasi moja karibu na uti wa mgongo.

Amesema baada ya kuingia madarakani kwa Rais Samia Suluhu Hassan, amekamatwa mara kadhaa, ikiwemo kukamatwa Mbeya mwaka 2024 na baadaye kukamatwa tena nyumbani kwake kabla ya maandamano yaliyopangwa na CHADEMA.

Lissu amesema kesi ya uhaini inayomkabili sasa ni sehemu ya historia hiyo.

“Utetezi wangu ni kwamba hii kesi ni kesi ya uongo unaofanywa na waendesha mashtaka na polisi,” amesema Lissu.