Uchunguzi kuhusu aliyekuwa kiongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuhusu madai ya ubadhirifu wa $138 milioni.
Uchunguzi wa mahakama umeanzishwa baada ya uchunguzi wa vyombo vya habari na nyaraka kumshutumu rais wa zamani wa DR Congo Joseph Kabila na familia yake kwa kunyakua dola milioni 138 za serikali, chanzo cha mahakama kilisema Jumatano.
Uchunguzi huo uliopewa jina “Congo Hold-Up”, na kuendeshwa na vyombo vya habari vya kimataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayopinga ufisadi umeibua hasira kati ya wananchi humo katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati.
Uchunguzi unamtuhumu Kabila, ambaye alitawala nchi hiyo kutoka 2001 hadi 2019 kwa ubadhirifu wa pesa kati ya 2013 na 2018.
Msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema Jumatatu kwamba waziri wa sheria “alimwandikia mwendesha mashtaka mnamo Novemba 20,” siku moja baada ya uchunguzi kuanza kuchapishwa.
Waziri “alitoa amri kwa madhumuni ya uchunguzi na mashtaka,” Muyaya alisema.
“Sisi kama serikali hatuwezi kukaa kando baada ya tuhuma hizo kuibuliwa”
Chanzo katika ofisi ya mwendesha mashtaka katika Mahakama ya Cassation ikiwa ndio mamlaka kuu ya mahakama kilisema Jumatano kwamba “uchunguzi wa mahakama umefunguliwa” kufuatia ombi la waziri wa sheria.
Uchunguzi huo unakuja baada ya chombo cha habari cha uchunguzi cha Ufaransa cha Mediapart na Jukwaa la Kulinda Watoa taarifa kutoka Afrika, kupata hati milioni 3.5 kutoka Benki ya Kimataifa ya Gabon na Ufaransa (BGFI).
Vyombo vya habari kumi na tisa na mashirika matano yasiyo ya kiserikali yanayoratibiwa na Jumuiya ya Upelelezi ya Ulaya (EIC) yalitumia muda wa miezi sita kusoma nyaraka hizo.
“Nyaraka zinaonyesha kuwa rais wa zamani Kabila, familia yake na jamaa walipokea, kwa ushirikiano wa benki ya BGFI, angalau dola milioni 138 kutoka kwa hazina ya serikali kati ya 2013 na 2018,” Mediapart ilisema.
Uchunguzi ulibaini kuwa pesa hizo zilitwaliwa “kupitia kampuni bandia.”
Ofisi ya vyombo vya habari ya Kabila katika taarifa ilikataa “mashtaka ya uwongo” na kushambulia “unyanyasaji usio na msingi kutoka kwa mamlaka fulani ambayo imejificha nyuma ya vyombo vya habari.”
Benki ya BGFI, kutoka makao makuu yake katika mji mkuu wa Gabon Libreville, ilisema katika taarifa yake siku ya Jumatano kwamba “imelaani vitendo vilivyo kinyume na sheria na maadili ambavyo huenda vilifanywa siku za nyuma ndani ya kampuni tanzu ya BGFI Bank RDC SA,” tawi la benki hiyo la Congo.