Heche: Lissu Hakutuambia Njia za Kuhamasisha Uasi

Shahidi wa tano wa upande wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, John Heche, ameiambia Mahakama Kuu kuwa licha ya kumsikia Lissu akizungumzia kuzuia na kuvuruga uchaguzi pamoja na kuhamasisha uasi, hakuwahi kuwaambia wao kama wafuasi au viongozi wa chama njia za kutekeleza kauli hizo.
Heche: Lissu Hakutuambia Njia za Kuhamasisha Uasi

Heche, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, ametoa kauli hiyo leo Septemba 15, 2026, wakati akihojiwa kwa maswali ya dodoso na Wakili Mkuu wa Serikali, Nassoro Katuga, katika kesi hiyo inayosikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.Katika sehemu ya ushahidi wake, Heche alikiri kwamba aliisikiliza hotuba ya Lissu iliyotolewa Aprili 3, 2025 na kwamba alimsikia Mwenyekiti huyo akizungumza kuhusu kuzuia uchaguzi. Hata hivyo, alipotakiwa kueleza kama Lissu aliwapa maelekezo ya namna ya kutekeleza hatua hizo, alisema hakuwahi kutoa maelekezo hayo.Katuga alimuuliza Heche kama Lissu aliwaambia njia za kuvuruga uchaguzi, kuzuia uchaguzi au kuhamasisha uasi. Katika maswali hayo, Heche alijibu mara kadhaa kuwa Lissu hakuwapa maelekezo hayo.Kwa upande mwingine, Heche alikiri kumsikia Lissu akisema “tutazuia uchaguzi”, huku pia akisema alimsikia akizungumza kuhusu kuvuruga uchaguzi na kuhamasisha uasi. Alikiri pia kumsikia Lissu akisema “mahakamani hakuendeki” na kwamba polisi wanaingiza kura feki.Hata hivyo, katika sehemu nyingine ya maswali, Heche alisisitiza kwamba kauli hizo hazikuambatana na maelekezo ya namna ya kuzitekeleza.Wakili Katuga pia alimuuliza Heche kuhusu msimamo wa CHADEMA wa “No Reforms No Elections”, ambapo shahidi alikiri kuwa huo ulikuwa msimamo wa chama. Heche alisema msimamo huo ulihusisha kutoshiriki uchaguzi hadi yafanyike mabadiliko, huku akisisitiza kuwa chama hicho kinaamini uchaguzi unapaswa kuwa huru na wa haki.Katika hatua nyingine, Katuga alimuuliza Heche kuhusu uchaguzi wa mwaka 2015 na iwapo ulikuwa huru na wa haki. Heche alisema uchaguzi huo ulikuwa na “figisu nyingi” na kwamba haukuwa huru wala wa haki. Alipoulizwa iwapo alikubali matokeo ya uchaguzi huo katika jimbo lake, alisema walikubali lakini uchaguzi ulikuwa na makosa mengi.Katuga aliendelea kumuuliza Heche iwapo, kwa kuwa alichaguliwa katika uchaguzi ambao yeye mwenyewe aliueleza kuwa haukuwa huru na wa haki, alikuwa na uwezo wa kukataa kutangazwa mshindi. Heche alisema hakuwa na uwezo huo.Mjadala huo uliingia pia katika suala la Tume ya Uchaguzi. Heche alieleza kuwa kwa mujibu wa Katiba, Tume ya Uchaguzi ndiyo yenye jukumu la kutangaza tarehe ya uchaguzi na kwamba haipaswi kuingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yake. Alipotakiwa kutaja ibara ya Katiba inayohusiana na suala hilo, alitaja Ibara ya 74.Katika ushahidi wake, Heche pia alikiri kwamba yeye, Lissu na wengine walikwenda Nairobi, Kenya, ambako walikutana na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga. Hata hivyo, alipoulizwa iwapo walikwenda kumwambia Odinga kwamba walikuwa wanakwenda kuzuia uchaguzi, kuhamasisha uasi, kuvuruga uchaguzi au “kukinukisha”, Heche alijibu kuwa hakukuwa na uasi dhidi ya nchi.Sehemu nyingine iliyozua mjadala Mahakamani ilikuwa kuhusu taarifa ambazo Heche alitoa kupitia vyombo vya habari, hususan East Africa Radio. Katuga alitaka shahidi akumbushwe baadhi ya kauli alizowahi kutoa, baada ya Heche kusema hakumbuki.Hapo Lissu, anayejitetea mwenyewe katika kesi hiyo, aliibua pingamizi akisema upande wa mashtaka haupaswi kumkumbusha shahidi ushahidi wake kwa namna iliyokuwa ikiombwa, akirejea vifungu vya Sheria ya Ushahidi. Lissu alidai kuwa iwapo shahidi anahitaji kukumbushwa alichokisema, utaratibu wa kisheria unapaswa kufuatwa.Mahakama hata hivyo iliruhusu shahidi kukumbushwa kuhusu video aliyowahi kuzungumza katika kituo cha East Africa Radio, na maswali ya Katuga yakaendelea.Katika sehemu hiyo, Heche alikiri kuwa aliwahi kuzungumza na kituo hicho mara nyingi, lakini alipoulizwa lini alitoa baadhi ya kauli zilizokuwa zikirejelewa, alisema hakumbuki.Katuga pia alimuuliza Heche kuhusu Tume ya Uchunguzi ya matukio ya Oktoba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji mstaafu Mohamed Chande.

Heche alisema hana kumbukumbu kwamba CHADEMA iliitwa na tume hiyo kutoa maoni, huku pia akisema yeye binafsi hakuitwa.Katika maswali mengine, Katuga alimuuliza Heche iwapo anafahamu kwamba kuchoma vituo vya kupigia kura ni uasi. Heche hakukubaliana na kauli hiyo. Alipoulizwa uasi ni nini, alijibu kuwa ni “kupinga, kukataa”.Katuga alipoendelea kumuuliza kuhusu vituo vya kupigia kura, Heche alisema vituo hivyo vinasimamiwa na Tume na kwamba endapo kituo kingechomwa, kosa hilo lingekuwa dhidi ya Tume.Heche alipoelezwa na Katuga kwamba katika hotuba hiyo Lissu kama aliwaambia watu njia za kuvuruga uchaguzi, kuzuia uchaguzi au kuhamasisha uasi, alijibu kuwa hakuwahi kuwaambia njia hizo.Kwa hiyo, licha ya Heche kukiri kwamba alimsikia Lissu akitumia baadhi ya maneno yanayodaiwa kuwa sehemu ya msingi wa mashtaka, shahidi huyo alisema hakusikia maelekezo ya namna ya kuyatekeleza.Katika sehemu nyingine ya ushahidi, Katuga alimuuliza Heche kuhusu aina ya uhaini ambayo Lissu anashtakiwa nayo. Heche alisema anafahamu kuwa ni “kuitishia Serikali na kuchapisha”, na alikiri pia kwamba anajua Lissu anashtakiwa kwa kutoa na kuchapisha maneno kwa nia ya kuitishia Serikali.Tundu Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma, baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa CHADEMA uliokuwa sehemu ya kampeni ya “No Reforms, No Election”. Siku iliyofuata, Aprili 10, 2025, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini, chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Toleo la 2023. Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, shtaka hilo linahusishwa na kauli anazodaiwa kutoa Aprili 3, 2025 katika mkutano wa CHADEMA Dar es Salaam kuhusu msimamo wa chama wa kuzuia uchaguzi wa mwaka 2025, kuhamasisha uasi na kuvuruga uchaguzi. Baada ya upande wa mashtaka kumaliza ushahidi wake, Mahakama Kuu iliamua Agosti 21, 2026 kwamba Lissu ana kesi ya kujibu, hatua iliyomlazimisha kuanza kutoa utetezi wake. Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.