Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai, anatazamiwa kutoa ushahidi wake wa utetezi dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, siku ya Ijumaa, Septemba 18, 2026.

Hatua hiyo imefikiwa leo September 16,2026, baada ya shahidi wa tano wa upande wa utetezi, John Heche, kumaliza kutoa ushahidi wake uliodumu kwa siku sita mbele ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Baada ya Heche kumaliza ushahidi wake, Lissu aliiambia Mahakama kuwa amefanya mawasiliano na Msajili wa Mahakama kuhusu utekelezaji wa wito kwa mashahidi watatu ambao mahakama iliamuru waitwe kutoa ushahidi katika kesi hiyo.
Mashahidi hao ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania(CDF).Generali Jacob Mkunda, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP. Camilius Wambura na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai DCI Ramadhani Kingai
“Waheshimiwa majaji, baada ya maelekezo ya Mahakama, nimewasiliana na Msajili wa Mahakama hii ambaye ameniletea taarifa ya utekelezaji wa amri ya Mahakama,” alisema Lissu.
Alisema Msajili amemueleza kuwa mashahidi wote watatu walioelekezwa wito Dodoma walipatikana, lakini haikufanikiwa kuwapatia nakala za wito kwa kuwa wote walidaiwa kuwa nje ya nchi.
Lissu alisema mmoja wa mashahidi hao, DCI Kingai, anatarajiwa kurejea nchini leo, huku Msajili akiahidi kuwa siku ya Ijumaa Kamishna wa Polisi DCI Kingai atakuwepo mahakamani kwa ajili ya kutekeleza wito wa Mahakama.
“Wale wawili ambao ni Jenerali Mkunda na IGP Wambura, haijulikani watarudi lini,” alisema.
Lissu aliomba Mahakama iahirishe kesi hiyo hadi Ijumaa saa 8:00 mchana, akisema muda wa asubuhi atautumia kumuandaa Kingai, ikiwa ni pamoja na kuchukua maelezo yake.
“Kuhusiana na waliobaki, itabidi tuendelee na huyu aliyeko halafu tutafanya maamuzi juu ya hawa wasiokuwepo,” alisema.
Lissu pia alisema anafahamu ratiba ya kesi hiyo na anatamani kesi ikamilike ili pande zote ziende kwenye hatua ya mwisho ya kutoa hoja za mwisho (final submissions).
“Kwa hiyo kama watakuwa wanakuja basi hatutachukua muda mrefu. Na wasipokuja kabisa, maana yake itakuwa ni juu ya Mahakama,” alisema Lissu.
Kwa upande wake, Wakili wa Jamhuri, Nassoro Katuga, alisema upande wa mashtaka hauna pingamizi dhidi ya ombi la kuahirishwa kwa kesi hiyo, ingawa uliomba Lissu ahakikishe mashahidi wake wanapatikana kwa wakati.
“Tumesikia mshtakiwa. Kwa masikitiko hatuna pingamizi, lakini hatupingi ombi la kuahirisha. Tunaiomba Mahakama hii basi mshtakiwa asisitize mashahidi wake waje kwa wakati,” alisema Katuga.
Baada ya kusikiliza hoja hizo,
Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa, Septemba 18, 2026, saa 8:00 mchana.
Awali kabla ya hoja hiyo Heche ambaye ni shahidi wa tano alimaliza ushahidi wake baada ya Lissu kumuuliza maswali ya mwisho ya kusawazisha yaliyohusu ripoti ya waangalizi wa SADC, mikutano ya Chadema, uchaguzi wa Tarime, uchaguzi wa Butiama, Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uchaguzi iliyoongozwa na Jaji mstaafu Othman Chande, pamoja na mapendekezo ya chama kuhusu sheria za uchaguzi.
Katika sehemu ya mwisho ya ushahidi wake, Heche alithibitisha kuwa ripoti ya waangalizi wa SADC ina masuala yanayohusu utekaji.
Lissu pia alimhoji kuhusu majibu aliyoyatoa awali kuhusu kauli zinazohusishwa na uasi, kuvuruga uchaguzi na kubadilisha mifumo ya uchaguzi. Heche alisema alichomaanisha ni kwamba maudhui ya kauli hizo yalikuwa yale yale yaliyohusu kubadilisha mifumo ya uchaguzi.
Kuhusu uchaguzi wa Tarime, Heche alisisitiza kuwa hakuwa na uwezo wa kukataa baada ya kutangazwa mshindi kwa sababu mamlaka ya kumtangaza mbunge yalikuwa kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi.
Katika hoja kuhusu Tume ya Chande, Heche alisema binafsi hajawahi kupokea mwaliko wowote wa kwenda kutoa ushahidi au maoni mbele ya Tume hiyo, licha ya Lissu kumuuliza kuhusu barua mbalimbali za mwaliko zilizowahi kutolewa.
Kuhusu mapendekezo ya Chadema kuhusu sheria za uchaguzi, Heche alisema chama kilipendekeza Tume ya Uchaguzi kuwa na watumishi wake kuanzia ngazi za juu hadi chini, badala ya usimamizi wa uchaguzi kuendelea kutegemea watumishi wa umma kama ilivyoelezwa mahakamani.
Heche pia alieleza kuwa Thabo Mbeki Foundation ni taasisi ya kimataifa kwa sababu inafanya kazi katika nchi zaidi ya moja.
Baada ya majibu hayo, Lissu alisema: “Waheshimiwa majaji, nimemaliza,” na hivyo kukamilisha ushahidi wa shahidi huyo wa tano wa upande wa utetezi.
Kesi hiyo inahusu shtaka la uhaini linalomkabili Lissu, ambaye anadaiwa kutenda kosa la kuitishia Serikali kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma, wakati wa kampeni ya Chadema ya “No Reforms, No Election” na amekana mashtaka yanayomkabili.