Vikosi vya usalama vya Sudan vimewaachia wanahabari wawili wa kituo cha televisheni cha Asharq ya Saudi Arabia, siku moja baada ya kuwaweka kizuizini huku ghasia mbaya zikizuka wakati wa maandamano mapya dhidi ya serikali ya kijeshi, kituo hicho kimesema Ijumaa.
Wakati wa maandamano ya Alhamisi ndani na karibu na Khartoum, “maafisa usalama watano waliovalia sare” waliwashikilia waandishi wa habari Maha al-Talb na Sally Othman na wengine katika ofisi zao kwa saa kadhaa, kituo hicho kilisema.
Sudan imekumbwa na msukosuko tangu kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan kuongoza mapinduzi Oktoba 25 na kumzuilia Waziri Mkuu Abdalla Hamdok.
Hamdok alirejeshwa kazini mnamo Novemba 21, lakini maandamano makubwa yameendelea huku waandamanaji wakikosa imani na ahadi za Burhan za kutaka kuiongoza nchi kuelekea demokrasia kamili.
Waandamanaji wanadai kuwa makubaliano hayo yanalenga tu kuhalalisha matendo ya majenerali, ambao wanawatuhumu kwa kujaribu kuendeleza utawala uliojengwa na aliyekuwa rais wa kiimla Omar al-Bashir, ambaye alipinduliwa mwaka 2019 kufuatia maandamano makubwa.
Katika mapigano mabaya zaidi ya barabarani tangu kurejea kwa Hamdok, waandamanaji watano waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa kwa risasi siku ya Alhamisi, ilisema Kamati huru ya Madaktari, ambayo ni sehemu ya vuguvugu la kuunga mkono upatikanaji wa demokrasia.
Mamlaka pia zilikata laini za simu na intaneti na kukandamiza vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na chaneli ya satelaiti inayofadhiliwa na Saudia ya Al-Arabiya.
Mwanahabari Othman alikatishwa na vyombo vya usalama katikati ya matangazo ya moja kwa moja na anasikika akisema kwenye video iliyosambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii: “Sitaweza kuendelea, mamlaka sasa inanikataza kuendelea na matangazo.”
Kamati ya Madaktari ilidai kwamba “uhalifu dhidi ya ubinadamu” ulifanyika mjini Omdurman, siku ya Alhamisi.
Kamati ilisema waandamanaji watano waliuawa kwa risasi kichwani au kifuani, na kwamba ambulensi zilizuiwa na angalau mtu mmoja aliyejeruhiwa vibaya alitolewa kwa nguvu kutoka kwa gari la wagonjwa na vikosi vya usalama.
Msemaji wa polisi alisema watu wanne walikufa katika machafuko ya Alhamisi na watu 297 walijeruhiwa, “wakiwemo maafisa 49 wa polisi.”
Pia alisema “magari matatu ya polisi yalichomwa moto” na kuwashutumu maandamano “viongozi wanaochukia vikosi vya usalama” kwa kutaka “kugeuza maandamano ya amani kuwa ghasia na makabiliano na vikosi vya usalama.”
Mapigano ya barabarani tangu mapinduzi ya Oktoba yamesababisha vifo vya watu 53 na kuwaacha mamia wakijeruhiwa, na wafuasi wa utawala wa kiraia nchini Sudan wameendelea kuitisha maandamano.