Serikali ya Nigeria siku ya Jumatano ilisema itaondoa marufuku iliyowekea mtando wa kijamii Twitter, miezi saba baada ya marufuku hiyo kuwekwa katika mzozo wa ujumbe wa Twitter wa Rais Muhammadu Buhari.
Nigeria ilisitisha shughuli za Twitter mwezi Juni baada ya kampuni hiyo kufuta ujumbe wa Rais Buhari, na kusababisha malalamiko ya kimataifa kuhusu uhuru wa kujieleza.
Serikali na kampuni ya Twitter zimekuwa katika mazungumzo juu ya kurejesha huduma hiyo kwa kuzingatia masharti kadhaa, ikiwa ni pamoja na Twitter kusajili shughuli zake nchini Nigeria.
“Serikali ya Shirikisho ya Nigeria inanielekeza niutaarifu umma kwamba Rais Muhammadu Buhari… ameidhinisha kuondolewa kwa marufuku iliyowekewa Twitter nchini Nigeria kuanzia saa 6 asubuhi leo,” taarifa kutoka kwa wakala wa maendeleo ya teknolojia ya habari nchini humo ilisema.
Watu wengi katika mji mkuu wa Nigeria wa Lagos walishindwa kupata huduma za Twitter hadi saa 6:30 asubuhi (2330 GMT), mwandishi wa habari wa AFP alisema.
Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Kashifu Inuwa Abdullahi, ambaye pia alikuwa kwenye kamati ya mazungumzo na Twitter, alisema kampuni hiyo kubwa ya mtandao wa kijamii imekubali kanuni za kurejesha huduma zake nchini humo.
Ikiwemo kuanzisha huluki ya kisheria nchini Nigeria, kuteua mwakilishi wa nchi na kutii majukumu ya kodi.
Twitter haikutoa maoni yao kuhusu masharti hayo.
Lakini ilisema marufuku hiyo ilizua wasiwasi mkubwa na kusema kuwa matumizi ya mtandao ni haki ya msingi kwa mwanadamu yeyote yule.
Marufuku hiyo iliwashangaza wengi nchini Nigeria, ambapo Twitter hutumika sana kwenye mawasiliano na ilichangia misukumo ya kisiasa na kudai haki kama vile #BringBackOurGirls baada ya Boko Haram kuwateka nyara takriban wasichana 300 wa shule mwaka 2014, na #EndSARS wakati wa maandamano ya kupinga ukatili wa polisi mwaka 2020.