Mahakama ya juu zaidi nchini Kenya ilianza kusikiliza kesi kuhusu mabadiliko ya katiba maarufu BBI, miezi michache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mwezi Agosti.
Uamuzi wa Mahakama kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya katiba, yanatarajiwa kutolewa baada ya siku tatu wiki hii, uamuzi ambao huenda ukawa na madhara makubwa katika uchaguzi wa rais na wabunge wa Agosti 9.
Serikali inataka kubatilisha maamuzi ya awali ya mahakama yaliyotupilia mbali mageuzi hayo makubwa na ambayo pia yalitajwa kuwa kinyume cha katiba. Maamuzi hayo yalikuwa pigo kwa Rais Uhuru Kenyatta na washirika wake.
Mpango huo wa BBI au Building Bridges Initiative (BBI) unalenga kubadili mfumo wa uchaguzi ambao umelaumiwa kwa ghasia za mara kwa mara nchini humo.
Lakini wapinzani wa Kenyatta wanaona kuwa mpango wa BBI utatoa nafasi kwake yeye kuendelea kuwa uongozini kwani mpango huo utampa nafasi ya kuwania wadhfa mpya wa Waziri mkuu hata baada ya yeye kuhudumu kwa awamu mbili kama rais wa nchi.
BBI iliundwa kufuatia makubiliano kati ya Kenyatta na mpinzani wake wa zamani Raila Odinga katika kile kilichoitwa “Handshake”. Makubaliano hayo yalitarajiwa kusitisha machafuko ya mara kwa mara kama yale ya baada ya uchaguzi wa 2017 na kusababisha vifo vya makumi ya watu.
Marekebisho yaliyopendekezwa ya katiba ya 2010 yaliidhinishwa na bunge mwezi Mei mwaka jana na yalipaswa kupigiwa kura ya maoni.
Lakini siku mbili tu baadaye, Mahakama Kuu ya Nairobi iliamua kuwa mabadiliko hayo hayakuwa halali kwa vile rais hakuwa na haki ya kuanzisha mchakato huo.
Mahakama ya Rufaa ya Kenya mwezi Agosti ilikubali maoni hayo na kusema Rais Uhuru Kenyatta anaweza hata kushtakiwa katika mahakama ya kiraia kwa kuanzisha mchakato huo.