Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne ulisema watu 32, wakiwemo wanawake na watoto, wameuawa wakati wa mashambulizi ya silaha katika eneo la Sudan Kusini lililokumbwa na ghasia za kikabila
Mashambulizi hayo katika vijiji viwili katika Jimbo la Jonglei mnamo Januari 23 yalipelekea raia kukimbia huku vijana wenye silaha kutoka kabila pinzani wakifyatua risasi na kuteketeza mali.
Miongoni mwa waliofariki ni watoto watatu waliozama kwenye mto walipokuwa wakijaribu kutoroka, Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) ilisema.
Takriban watu 26 walijeruhiwa, wakiwemo wanawake na watoto, na wengine hawajulikani walipo kwa siku mbili sasa baada ya umwagaji damu katika eneo la Baidit.
“UNMISS inalaani vikali shambulio hilo dhidi ya raia na inataka makundi na watu binafsi kuchukua hatua za haraka ili kuepusha ongezeko zaidi la machafuko ambalo litahatarisha maisha ya watu zaidi.”
Ujumbe huo pia unatoa wito kwa mamlaka kufanya uchunguzi kwa wakati na kwamba wahusika wawajibishwe kwa matendo yao.”
Ujumbe wa kulinda amani ulitumwa kufanya kazi kwa mwaka mmoja mwaka 2011 wakati Sudan Kusini ilipopata uhuru, lakini mamlaka yake yameongezwa mara kwa mara huku nchi hiyo changa ikiteseka kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe na viwango vya juu vya ghasia za kikabila.
Zaidi ya watu 700 waliuawa na wengine kubakwa na kutekwa nyara huko Jonglei kati ya Januari na Agosti 2020 katika uvamizi uliofanywa na wanamgambo wa kikabila katika jimbo la mashariki mwa nchi.
Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa uligundua kuwa viongozi wa kisiasa na kijeshi walihusika katika ghasia ambapo wanamgambo walivamia vijiji katika mashambulizi yaliyoratibiwa dhidi ya wapinzani wao, wakitumia mapanga, bunduki na wakati mwingine maguruneti ya kurushwa kwa roketi.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, Nicholas Haysom, aliliambia Baraza la Usalama mwezi Disemba kwamba idadi ya majeruhi kutokana na ghasia za ndani kote nchini humo imepungua kwa takriban nusu katika mwaka 2021 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Lakini ukosefu wa usalama unaendelea kutanda, huku serikali ya muungano ikishindwa kukomesha ghasia au kuwaadhibu wahusika wa ghasia hizo karibu miaka miwili baada ya kuchukua mamlaka huko Juba.
Rais Salva Kiir na naibu wake ambaye pia ni hasimu wake wa muda mrefu, Riek Machar, waliunda serikali na kugawana madaraka mwaka 2020 baada ya miaka mingi ya umwagaji damu kati ya vikosi vyao na kusababisha karibu watu 400,000 kupoteza maisha.
Lakini serikali ni dhaifu na ina imani haba, na Umoja wa Mataifa umeonya kwamba makubaliano ya amani yako katika hatari ya kusambaratika ikiwa nguzo muhimu za mapatano hayo hazitatekelezwa.