Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Kenya: Mwanafunzi acharazwa viboko kwa kula chapati nyingi - Mwanzo TV

Kenya: Mwanafunzi acharazwa viboko kwa kula chapati nyingi

Mwanafunzi mmoja raia wa Kenya amelazwa katika hospitali moja mjini Mombasa baada ya kuchapwa viboko kwa kula chapati tano badala ya ile aliyopewa na shule.

Bw Fredrick Ngure mzazi wa mvulana huyo alipokea simu kutoka shuleni na kuambiwa kuwa mwanawe alikuwa mgonjwa na kwamba lazima amkimbize hospitalini.

Aliendesha gari haraka hadi shule ya Gremon iliyoko Bamburi, Kaunti ya Mombasa, na kumpata mwanawe wa miaka 13 akiwa na majeraha mwili mzima.

“Mwanangu alipigwa kama mwizi kwa sababu tu alikula chapati za ziada mnamo Januari 23. Alifungiwa ndani ya chumba, akapigwa na mkurugenzi na wanafunzi wengine baada ya kula chapati tano.”

Walimu wameshutumiwa kwa kumpiga mvulana huyo kwa kutumia bomba lakini uongozi wa shule umewalaumu wanafunzi wenzake.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani na video zinazosambazwa mitandaoni, mvulana huyo mwenye umri wa miaka 13 ana alama nyeusi mwilini mwake.

Polisi kutoka eneo la Kadzandani, Nyali, wanamshikilia mwalimu mkuu wa shule hiyo ya kibinafsi kuhusiana na shambulio hilo.

Mshukiwa mwingine ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne angali anasakwa na wapelelezi.

Naibu mkuu wa polisi wa Nyali Ibrahim Dafallah alisema wanachunguza shambulio hilo.

Wazazi wake wanasema shule haikuwaarifu kuhusu tukio hilo hadi wiki moja baadaye mvulana huyo alipougua.

Bw Ngure alisema familia yake haitalegea hadi waliohusika kwenye tuko hilo waadhibiwe.

“Uongozi wa shule ulifanya makosa kumkabidhi mwanangu kwa wanafunzi wenzake ili wamwadhibu.”

“Alipigwa na kufungiwa bwenini kwa muda wa wiki nzima na hakwenda darasani.”

Madaktari katika hospitali ya Coast General alikopelekwa  wanasema mvulana huyo ana jeraha kwenye figo na majeraha mengine katika sehemu zake za siri.

Maafisa wa elimu wa eneo hilo wamefunga shule hiyo baada ya ukaguzi uliofuatia tukio hilo.