Takriban watu milioni 13 nchini Kenya, Somalia na Ethiopia wanakabiliwa na njaa kali huku Pembe ya Afrika ikikumbwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilisema Jumanne.
Mvua haijanyesha katika misimu ya mvua mitatu mfululizo huku eneo hilo likishuhudia hali ya ukame mbaya zaidi tangu 1981, shirika la Umoja wa Mataifa lilisema.
Ukame huo umeharibu mazao na kusababisha vifo vingi vya mifugo na kuwalazimu familia za vijijini zinazotegemea ufugaji na ukulima kuacha makazi yao.
Maji na ardhi ya malisho ya wanyama ni haba na utabiri wa mvua katika nchi hizi unatishia maafa zaidi, alisema Michael Dunford, mkurugenzi wa WFP Afrika Mashariki.
“Mavuno yanaharibiwa, mifugo inakufa, na njaa inaongezeka kwani ukame wa mara kwa mara unaathiri Pembe ya Afrika,” alisema katika taarifa yake.
“Hali hiyo inahitaji hatua za haraka za kibinadamu” ili kuepuka kujirudia kwa janga kama lile la Somalia mwaka 2011, wakati watu 250,000 walikufa kwa njaa kutokana na ukame wa muda mrefu.
Msaada wa chakula unasambazwa katika eneo kame la Kenya, Ethiopia na Somalia ambako viwango vya utapiamlo viko juu na baadhi ya watu milioni 13 wako katika hatari ya njaa kali katika robo ya kwanza ya mwaka huu.
Watu milioni 5.7 wanahitaji msaada wa chakula kusini na kusini-mashariki mwa Ethiopia, ikiwa ni pamoja na watoto nusu milioni wenye utapiamlo.
Nchini Somalia, idadi ya watu wanaotajwa kuwa na njaa kali wanatarajiwa kuongezeka kutoka milioni 3.5 hadi milioni 4.6 ifikapo Mei iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
Watu wengine milioni 2.8 wanahitaji msaada kusini-mashariki na kaskazini mwa Kenya, ambapo dharura ya ukame ilitangazwa mnamo Septemba.
WFP ilisema dola milioni 327 zilihitajika kutatua mahitaji ya haraka katika kipindi cha miezi sita ijayo na kusaidia jamii za wafugaji kuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.