Ajali ya basi kwenye barabara kuu katikati mwa Sudan siku ya Jumatano ilisababisha vifo vya takriban watu 10 na kuacha kadhaa wakiwa wamejeruhiwa, mamlaka ilisema.
Ajali hiyo ilihusisha mabasi mawili na ilifanyika katika wilaya ya Bara katika jimbo la Kordofan Kaskazini.
“Watu kumi waliuawa na wengine 30 kujeruhiwa, wengine vibaya, kutokana na ajali hiyo… katika eneo la Bara,” polisi walisema katika taarifa.
Ajali hiyo huenda ilisababishwa na mwendo kasi uliopelekea kugongana na kusababisha moja ya mabasi hayo kupinduka, waliongeza.
Sudan imekuwa ikitatizika kwa muda mrefu kutokana na barabara mbovu na miundombinu duni, ambayo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa inatokana na mzozo wa kiuchumi unaozidi kuwa mbaya.
Takwimu za hivi punde za Shirika la Afya Duniani na Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa vifo vya barabarani nchini Sudan vimefikia takriban 10,000 kila mwaka kati ya 2016 na 2019. Mgogoro wa kiuchumi wa nchi hiyo ulizidishwa na mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana yaliyoongozwa na jenerali Abdel Fattah al-Burhan.