Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Historia ya Ukraine na Urusi na vita vinavyoendelea - Mwanzo TV

Historia ya Ukraine na Urusi na vita vinavyoendelea

Hata kabla ya Urusi kuvamia Ukraine mataifa hayo mawili yamekuwa na historia ndefu ya migogoro.

Historia na utamaduni wa Urusi na Ukraine unafanana- wanashiriki dini moja ya Kikristo ya Orthodox, na lugha zao, mila na vyakula vya kitaifa vinafanana.

Ukraine inaonekana na Warusi wengi kama ‘ndugu mdogo’ wa taifa lao na wanapaswa kuishi ipasavyo.

Tuangalie historia ya Ukraine

1922 hadi 1991

Ukraine ilikuwa sehemu ya Urusi kuanzia 1922 hadi 1991 wakati Moscow ilikuwa mji mkuu wa USSR au Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti.

Muungano huo ulijulikana pia kama Umoja wa Kisovieti (SU).

Orodha ya nchi zilizokuwa sehemu ya USSR: Muungano wa Kisovyeti

Armenia

Azerbaijan

Belorussia sasa Belarus

Estonia

Georgia

Kazakhstan

Kirgiziya sasa Kyrgyzstan

Latvia

Lithuania

Moldavia sasa Moldova

Russia

Tajikistan

Turkmenistan

Ukraine

Uzbekistan

USSR ilikuwa nchi kubwa zaidi ulimwenguni wakati huo, ikiwa na ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba 22,402,200. Umoja wa Kisovieti ulikuwa nchi ya chama kimoja kilichotawaliwa na Chama cha Kikomunisti.

Vladimir Ulyanov maarufu kama Lenin, alihudumu kama mkuu wa kwanza na mwanzilishi wa serikali ya Urusi ya Kisovieti kuanzia 1917 hadi 1924 na mkuu wa Muungano wa Sovieti kuanzia 1922 hadi 1924. Chini ya utawala wake, Urusi, na baadaye Muungano wa Sovieti, ikawa nchi ya chama kimoja cha kisoshalisti iliyotawaliwa na Soviet Union.

Kiongozi mwingine wa muungano huo, Joseph Stalin, alishika madaraka kama Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Umoja wa Kisovieti (1922-1952) na alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Kisovieti (1941-1953).

Licha ya kutawala nchi kama sehemu ya uongozi wa pamoja, hatimaye aliunganisha mamlaka na kuwa dikteta wa Umoja wa Kisovyeti kufikia miaka ya 1930.

Mwaka wa 1932- 1933 Ukraine ilikumbwa na njaa kali katika kile kilichoitwa ‘Holodomor’. Mfumo huo ulikuwa mpango wa kuwaua wa Ukraine kwa kuwasababishia njaa kali. Waukraine milioni 7.2 waliuawa.

Mnamo Septemba 1934, nchi hiyo ilijiunga na League of Nations, shirika la kwanza la kiserikali ulimwenguni pote lililoanzishwa ili kudumisha amani ya ulimwengu.

Mnamo Desemba 14, 1939, Muungano wa Sovieti ulifurushwa kutoka muungano wa League of Nations kwa kuivamia Finland.

Mwanzo wa vita vya Baridi

Nikita Khrushchev, ambaye alikuwa katibu wa kwanza wa Chama cha Kikomunisti cha Umoja wa Kisovieti kuanzia 1953 hadi 1964, alishutumu mikakati ya Joseph Stalin.

Mnamo 1956, alianzisha mikakati ya kuondoa mfumo wa Stalin kwa kuendelea kurahisisha udhibiti wa chama cha ujamaa.

Katika miaka ya 1950 na 1960, USSR ilijenga sekta ya sayansi na teknolojia katika jaribio la kuonyesha ubabe kwa Amerika.

Kusambaratika kwa muungano wa USSR

Mnamo 1990, mataifa yaliyokuwa ndani ya muungano wa USSR ya Latvia na Estonia yalitangaza uhuru wao.

Mikhail Gorbachev, ambaye alikuwa katibu mkuu wakati huo, hakuweza kudhibiti maeneo yaliyokuwa mbali na Moscow.

Kufikia Desemba 1990, mataifa yote yaliyokuwa ndani ya muungano wa USSR yakajiondoa kutoka kwa muungano, Urusi na Kazakhstan zikasalia pamoja.

Ukraine, jamhuri ya pili kwa ukubwa katika muungano wa USSR, ilitangaza uhuru wake mnamo 1991 baada ya kufanya kura ya maoni kujiondoa kwa muungano.

Mwanzo wa mzozo kati ya Ukraine na Urusi

Kufuatia kutiwa saini kwa Mkataba wa 1994 wa Budapest juu ya Uhakikisho wa Usalama kati ya Amerika, Uingereza, na Urusi, pamoja na makubaliano sawa na Ufaransa na China, Ukraine ilikubali kuharibu silaha zake zote za nyuklia, na kujiunga na Mkataba wa Non Proliferation of Nuclear Weapons.

Kufikia 1996, Ukraine ilihamisha silaha zake zote kwa Urusi.

Mzozo mkubwa wa pili ulikuwa juu ya hatima ya meli katika bahari ya Black Sea pamoja na besi zake za kufanya kazi, haswa Sevastopol kwenye Peninsula ya Crimea.

Tamko la bunge la Urusi kwamba jimbo la Crimea liko chini ya Ukraine kinyume cha sheria liliibua mzozo mwingine mpya kati ya mataifa hayo huku wakipigania eneo la Peninsula ya Crimea.

Jamhuri huru ya Ukraine

Uchaguzi wa Rais ulifanyika nchini Ukraine tarehe 31 Oktoba, 21 Novemba na 26 Desemba 2004. Uchaguzi huo ulikuwa wa nne kufanyika katika nchi huru ya Ukraine baada ya taifa hilo kupata uhuru kutoka kwa Muungano wa Sovieti.

Viktor Yanukovych alishinda uchaguzi wa 2004, hesabu ilipofanywa upya mwaka wa 2005 Viktor Yushchenko akatangazwa kuwa rais wa tatu wa Ukraine.

Mnamo 2008, Muungano wa kujihami wa NATO uliahidi Ukraine na Georgia kuwa watajiunga na muungano huo.

Maandamano ya Euromaiden 2013

Maandamano ya Euromaiden yalikuwa wimbi la maandamano na machafuko ya kiraia nchini Ukraine, ambayo yalianza usiku wa Novemba 21, 2013 yakiwa maandamano ya umma huko Maidan Nezalezhnosti mjini Kyiv.

Maandamano hayo yalichochewa na uamuzi wa serikali ya Ukraine kusitisha utiaji saini wa Mkataba wa biashara kati ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya na Ukraine, badala yake ikachagua uhusiano wa karibu na Urusi na Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia.

Rais wa Nne wa Ukraine Viktor Yanukovych aondolewa madarakani

Rais wa zamani wa Ukraine Viktor Yanukovych

Kamati ya Rada ya Verkhovna ilipiga kura mnamo Februari 22, 2014 Wabunge walipiga kura ya ‘kumwondoa Viktor Yanukovych kutoka wadhifa wa rais wa Ukraine’ kwa msingi kwamba hakuweza kutekeleza majukumu yake na kufanya uchaguzi wa mapema wa rais mnamo Mei 25.

Ndani ya siku chache, watu wenye silaha waliteka bunge katika eneo la Ukraine la Crimea na kupandisha bendera ya Urusi. Moscow baadaye ikateka eneo hilo.

Kujitenga kwa Donbas

Mnamo Aprili 2014 Waasi wanaounga mkono Urusi katika eneo la mashariki la Donbass watangaza uhuru na kujitenga kutoka Ukraine.

Takriban watu 15,000 wauawa tangu katika mapigano kati ya wanaotaka kujitenga na jeshi la Ukraine, kulingana na serikali ya Kyiv.

Kufikia 2017 Makubaliano ya ushirika kati ya Ukraine na EU yafungua masoko kwa biashara huria ya bidhaa na huduma, na uwezo wa kusafiri bila visa kwa kwa raia wa Ukraine kwenda mataifa ya EU.

2019: Rais wa sasa Volodymyr Zelenskiy achaguliwa kuwa rais wa Ukraine.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy

Mwanzo wa vita; Urusi yaivamia Ukraine

Jan. 2021: Zelenskiy atoa wito kwa rais wa Amerika Joe Biden kuruhusu Ukraine kujiunga na muungano wa kujihami wa NATO. Mnamo Februari, serikali yake ilizuia mali ya kiongozi wa upinzani Viktor Medvedchuk, mshirika mashuhuri wa Kremlin nchini Ukraine.

2021: Urusi yaanza kukusanya wanajeshi karibu na mipaka ya Ukraine katika kile inachosema ni mazoezi na mafunzo kwa wanajeshi.

Novemba 2021: Picha za satelaiti zilizopigwa na Maxar Technologies zinaonyesha kuongezeka kwa vikosi vya Urusi karibu na Ukraine ikikadiriwa kuwa wanajeshi 100,000 wa Urusi wakiwa mpakani.

Desemba 17, 2021: Urusi yawasilisha madai ya usalama ikiwa ni pamoja na kwamba muungano wa NATO uondoe wanajeshi na silaha zake kutoka Ulaya mashariki na kuizuia Ukraine kujiunga na muungano huo.

Januari 24 2022: NATO yaweka vikosi vyake katika hali ya tahadhari na kuimarisha Ulaya mashariki kwa meli na ndege zaidi za kivita.

Januari 26: Washington yajibu matakwa ya usalama ya Urusi, ikirudia kujitolea kwa sera ya NATO kwa uwazi na mazungumzo huku ikitoa wito wa kutathmini wasiwasi wa Moscow kuhusiana na kuwepo kwa silaha za NATO Ulaya Mashariki.

Siku mbili baadaye Urusi inasema matakwa yake kwa NATO hayajashughulikiwa.

Februari 2022: Huku kukiwa na hofu ya nchi za Magharibi kwamba Urusi inaweza kushambulia Ukraine, Amerika ikasema itatuma wanajeshi 3,000 wa ziada kwa wanachama wa NATO ikiwa ni Poland na Romania.

Washington na washirika wake wakasema hawatatuma wanajeshi wake nchini Ukraine, lakini wakaonya kuhusu vikwazo vikali vya kiuchumi iwapo rais wa Urusi Vladimir Putin atachukua hatua za kijeshi.

Februari 21: Katika hotuba ya televisheni, Putin akasema Ukraine ni sehemu muhimu ya historia ya Urusi na ina utawala wa kibaraka unaosimamiwa na mataifa ya kigeni.

Putin aamuru kile alichokiita vikosi vya kulinda amani katika maeneo mawili yaliyojitenga mashariki mwa Ukraine, baada ya kuyatambua kuwa huru.

Februari 22: Amerika, Uingereza na washirika wao waiwekea vikwazo wabunge wa Urusi, benki na mali nyinginezo kwa kuitikia agizo la jeshi la Putin.

Ujerumani yasitisha mradi wa bomba la gesi la Nord Stream 2. Bomba ambalo husambaza gesi kutoka Ujerumani hadi Urusi.

Februari 23: Viongozi wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi waomba Urusi usaidizi wa kuzima uchokozi kutoka kwa jeshi la Ukraine.

Februari 24: Putin aidhinisha ‘operesheni maalum za kijeshi’ nchini Ukraine.

Vikosi vya Urusi vyanza mashambulio ya makombora na mizinga na kushambulia miji mikubwa ya Ukraine ikiwemo Kiev.